Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Jokate Mwegelo, amewataka vijana wa Tanzania kuwa daraja la kuunganisha watu na kuleta maendeleo, na si kuwa chanzo cha migogoro na vurugu kwenye jamii.
Akizungumza siku ya Jumamosi Aprili 19, 2025 kama mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya “Samia First Time Voters” uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jokate amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na kutumia nafasi zao kwa busara na tija

.
“Katika zama hizi vijana lazima tujiendeleze, tufanye siasa, tushike uchumi wetu ili tuwe na maamuzi yetu wenyewe. Hatutaki vijana wabeba ajenda za watu. Kila kijana awe daraja la maendeleo, si chanzo cha migogoro,” amesema Jokate.
Jokate amesisitiza kuwa vijana wa vyuo na vyuo vikuu wana nafasi kubwa katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2025, akieleza kuwa takribani kura milioni 6 mpya zinatarajiwa kupigwa na wapigakura wa mara ya kwanza, wengi wao wakiwa vijana wa elimu ya juu.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema kuwa vijana wana ari kubwa ya kuleta mabadiliko kwa kuchagua kiongozi anayekubalika na wananchi wote ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan.
“Twendeni tukamsemee Rais Samia mambo aliyoyafanya. Rais mwenye maono, mwenye huruma, mwenye dhamira ya kweli ya maendeleo ya vijana na taifa hili. Oktoba tunatakiwa kumrudishia imani yake,” amesema Zungu.

Naye Pascrates Albinus Mwemezi, Mwenyekiti wa UVCCM Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar es Salaam, amesema utafiti umeonesha kundi kubwa la wapigakura wa mara ya kwanza liko kwenye vyuo vikuu, wengi wao wakiwa hawakupiga kura mwaka 2020.
“Kwa takwimu tulizonazo, kundi la vyuo na vyuo vikuu lina wapigakura wengi wa mara ya kwanza. Ndio maana tumeamua kwa makusudi kuhamasisha kundi hili kupitia kampeni hii ya ‘Samia First Time Voters’,” amesema Mwemezi.
About The Author
Last modified: April 20, 2025