Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Wakulima jijini Arusha wamepongeza juhudi za Serikali katika kuwawezesha kuongeza tija kwa kutoa ruzuku na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Pongezi hizo zimetolewa na mkulima Alphonce Massaga, anayejishughulisha na kilimo cha mahindi katika Kata na Kijiji cha Laroi, wilaya ya Arusha Vijijini, alipotembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwenye maonesho kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Massaga amesema kuwa, ziara yake kwenye banda la TFRA imemwezesha kufahamu umuhimu wa kujisajili kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea, ambapo tayari amepata namba yake ya mkulima itakayomwezesha kununua mbolea na mbegu kwa bei ya ruzuku.
Aidha, amepata fursa ya kutembelea banda la Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), ambapo alijifunza jinsi ya kuchagua mbegu bora zinazofaa kwa shamba lake ili kuongeza uzalishaji.
Katika kuhakikisha wakulima wanapata huduma stahiki, watumishi wanawake wa TFRA wamejizatiti kutoa elimu na mwongozo sahihi kwa wakulima wanaotembelea banda hilo. Juhudi hizi ni sehemu ya maonesho yanayoelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yatakayofanyika tarehe 8 Machi 2025.
About The Author
Last modified: March 2, 2025