Visit Sponsor

Written by 7:53 am KITAIFA Views: 4

WAZIRI KABUDI:VYOMBO VYA HABARI NI MUHIMILI MUHIMU MAENDELEO

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI q Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amekutana na wadau wa sekta ya habari na utangazaji nchini katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 18 Desemba 2024. Katika mkutano huo, Waziri Kabudi alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kama mhimili muhimu wa maendeleo, umoja, na mshikamano wa kitaifa.

Profesa Kabudi alisema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuonyesha taswira halisi ya Tanzania ndani na nje ya mipaka yake. Alieleza kuwa mchango wa vyombo hivi umekuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, na kitamaduni, huku akisisitiza kuwa sekta ya habari ni nguzo muhimu ya ustawi wa taifa.

Akizungumzia juhudi za serikali katika kuboresha sekta hiyo, Waziri Kabudi alibainisha kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita kuimarisha mazingira ya uwekezaji kupitia dhana ya 4R inayosimamia Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi, na Ujenzi wa Taifa. Alisema, Serikali inaendelea kurekebisha sera zinazoongoza vyombo vya habari ili kuhakikisha sekta hii inakidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa na mazingira ya sasa. Hatua hizi zitatekelezwa mapema iwezekanavyo.

Waziri Kabudi pia aliwataka waandishi wa habari kudumisha maadili na weledi katika utendaji kazi wao. Alisisitiza umuhimu wa waandishi kujifunza taaluma mbalimbali ili wawe na uwezo wa kueleza kwa ufasaha na kuelimisha jamii. Aidha, alitangaza kuwa Bodi ya Ithibati ya inayosimamia misingi ya taaluma ya habari itazinduliwa rasmi mwezi Januari 2025, ambapo itaweka mkazo katika kutoa mafunzo, kusimamia maadili, na kulea taaluma ya uandishi wa habari kwa manufaa ya taifa.

Pamoja na juhudi za kuimarisha sekta hiyo, Waziri Kabudi aligusia changamoto zinazoikumba sekta ya habari, zikiwemo hali ngumu ya kiuchumi, mabadiliko ya teknolojia, na athari za teknolojia ya akili bandia (Artificial Intelligence). Alitoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuwekeza katika teknolojia za kisasa badala ya kusubiri mabadiliko yawakute bila maandalizi.

Aidha, Waziri Kabudi alibainisha changamoto za mikataba duni ya ajira, ukosefu wa bima ya afya, na mafao ya uzeeni kwa waandishi wa habari. Aliahidi kuwa wizara yake itashirikiana na NSSF pamoja na wizara nyingine husika kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mikataba yenye heshima na uzeeni wenye staha.

Waziri huyo pia aliwataka waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kuzingatia dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 na kutoa mchango wa maana katika kufanikisha malengo yake. “Vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa letu,” alisema Profesa Kabudi.

Na kusisitiza kuwa sekta ya habari inapaswa kupewa nafasi maalum katika ajenda ya maendeleo ya taifa. Alitoa wito kwa wadau wa sekta hiyo kushirikiana na serikali katika kuhakikisha vyombo vya habari vinaimarika na vinaendelea kuwa mhimili wa mshikamano, umoja, na maendeleo endelevu nchini Tanzania.

About The Author

(Visited 4 times, 1 visits today)

Last modified: December 19, 2024

Close