Visit Sponsor

Written by 12:45 pm KITAIFA Views: 9

KIKAO KAZI CHA WAKUU WA IDARA ZA UTAWALA NA RASILIMALIWATU SERIKALINI CHAIVA, KAIMU KATIBU MKUU-UTUMISHI AWAITA

Kaimu Katibu Mkuu, UTUMISHI, BW.Xavier Daudi akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma



Na Mwandishi Wetu-Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya  Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetoa wito kwa Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kushiriki Kikao Kazi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupata maelekezo kuhusu masuala yanayohusu Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika utumishi umma kwa kuzingatia shabaha na vipaumbele vya Taifa.



Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw.  Xavier Daudi amebainisha hayo leo Alhamisi Desemba 12, 2024 wakati akizungumza na  Waandishi wa Habari jijini hapa kuhusu kikao kazi hicho kitakachofanyika Desemba 17-19, mwaka huu mbapo amesema Washiriki wa kikao hicho ni kutoka kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika na  Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa  na Serikali za Mitaa.



Bw. Daudi amesema kupitia kikao hicho Wakuu hao watapata fursa ya  kubadilishana mawazo na maelekezo kuhusu vipaumbele vya serikali kwenye ajira, maandalizi ya ikama na bajeti ya mishahara kwa Watumishi wa Umma nchini.

Amesema wameitana kujadili masuala yanayojitokeza kwenye utekelezaji wa majukumu yao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.



“Malengo hasa ya kikao kazi hiki ni kubadilishana uzoefu, tunajua utumishi wa umma ni mpana sana na nchi yetu ni kubwa, wale wanaofanya vizuri wanaongea na wenzao na wanabadilishana zile changamoto ili tuwahudumie watanzania vizuri tunakumbushana mambo ya msingi maana tunajua sekta au wizara na taasisi mbalimbali zimekuwa na mabadiliko mengi hasa kwenye mifumo,”alisema.



Amesema kikao hicho kitatumika kupeana maelekezo ili kazi za serikali zifanyike vizuri kwenye maeneo yanayolegalega.





Naye, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ibrahim Mahumu, amesema moja ya maeneo ambayo watajadili ni maandalizi ya ikama ya bajeti ya mishahara, usimamizi wa rasilimaliwatu na namna ya kushughulikia malimbikizo ya mishahara.



“Kwenye usimamizi wa rasilimaliwatu, kuna eneo la usimamizi wa mishahara na baadhi ya changamoto zinakabili eneo hilo tunaweza kuongea na wenzetu kwa maana ya wasimamizi wa Rasilimaliwatu hasa kwenye eneo la uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu katika kushughulikia majukumu na haki mbalimbali za watumishi, tumeona yana changamoto na tunaweza kuwashirikisha na kutengeneza njia bora ya kuweza kutatua changamoto kwa watumishi wetu walioko taasisi mbalimbali za serikali,”amesema.





Kadhalika, amesema eneo la maandalizi ya ikama na bajeti ya mishahara litajadiliwa kutokana na kuwa na changamoto na Ofisi hiyo ndio yenye jukumu la kusimamia maandalizi hayo kwa watumishi wa umma.



“Tunaelekea kwenye mwisho wa mwaka huwa kuna maandalizi ya ikama na bajeti ya mishahara kwa hiyo kuna mambo mengi ya kuwekana sawa ili kwenye eneo hilo wanapoanza kubainisha mahitaji ya watumishi wanaopaswa kuajiriwa ni vizuri kupeana maeneo ya kipaumbele vya serikali ili kujua mahitaji yao na vipaumbele kuhusu aina ya watumishi wanaopaswa kuajiriwa kwa mwaka husika,”amesema.




Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma Serikalini,  Bi. Felister Shuli, amesema wakuu hao watajengewa uelewa namna ya kufanya kazi kwa ufanisi kusimamia rasilimaliwatu kwenye maeneo yao

About The Author

(Visited 9 times, 1 visits today)

Last modified: December 12, 2024

Close