Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Kwa Mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024, viashiria vya kiuchumi vinaonesha kwamba Kampuni ya UTT AMIS pamoja na Mifuko inayoisimamia imeendelea kufanya vizuri.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 15, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS Simon Migangala akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa Wawekezaji wa Mfuko wa Umoja (Umoja Fund) jijini Dar es Salaam.
Kwamba thamani ya Mifuko hiyo ambayo ni Umoja Fund, Wekeza Maisha, Jikimu, Liquid Fund na Bond Fund imeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 1.5354 Juni 30, 2023 hadi Shilingi Trilioni 2.2382 Juni 30, 2024.
“Hili ni ongezeko la Shilingi Bilioni 702.8, sawa na asilimia 45.7 ikilinganishwa na ongezeko la shilingi bilioni 538.9, sawa na asilimia 54.0 kwa mwaka uliopita,” amesema Migangala.
Migangala amebainisha kuwa ongezeko la ukubwa wa mifuko umetokana na faida iliyopatikana katika uwekezaji pamoja na ongezeko la la idadi ya wawekezaji 79,519, sawa na asilimia 32 waliojiunga katika mifuko kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na Wawekezaji 47,480, sawa na asilimia 24 waliojiunga mwaka wa fedha uliopita.
“Kama nilivyosema hapo awali, kwamba mifuko yote imetoa faida nzuri kwa wawekezaji wake. Faida kwa Mfuko wa Umoja ilikuwa asilimia 12.1,” ameongeza Migangala.
Akizungumzia kuhusu matarajio ya mwaka wa Fedha 2024/2025, Migangala amesema kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kampuni ya UTT AMIS ulioishia Juni, 30, 2024, umekuwa na mafanikio makubwa zaidi ya ilivyotarajiwa.
“Kwa mfano thamani ya mifuko ilikisiwa kukua kutoka shilingi bilioni 290.7 Juni 30, 2019 mpaka shilingi bilioni 485.9 kabla ya kurekebishwa na kuwa shilingi bilioni 1,007.9 Juni 30, 2024. Hata hivyo thamani halisi ya mifuko mpaka kufikia Juni 30, 2024 ilikuwa ni shilingi Trilioni 2.2 ambayo ni mara mbili ya kiwango kilichotarajiwa,” ameeleza Migangala.
Migangala amesema katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Mpango mpya, UTT AMIS inatarajia kukamilisha uboreshaji wa mifumo kama msingi wa kukuza biashara yake.
About The Author
Last modified: November 16, 2024