Visit Sponsor

Written by 6:58 am BIASHARA Views: 6

ZRA YASHAURI WAHARIRI KUWAJENGEA UWELEDI WAANDISHI

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI

-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Zanzibar (ZRA), imewashauri Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kuwajengea waandishi wao uweledi wa kuchagua tahsusi maalum ili  kuripoti kitaalamu hususan katika masuala ya mapato.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi kutoka ZRA, Makame Khamis Mohamed wakati akitoa salamu za mamlaka hiyo katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika ukumbi wa NSSF Dar es Salaam kwa siku tatu.

Alisema kwa bahati mbaya, Tanzania wapo waandishi waliochagua maeneo na kubobea kwayo, basi ni wachache, hivyo, alitoa rai kwa Wahariri kuwasaidia waandishi wao kujikita katika kutambua na kuripoti kwa uweledi katika eneo muhimu la kodi na mapato.

Aliongeza kuwa, kujikita katika tahsusi maalum, kujifunza na kuijua kikamilifu taaluma ya Kodi, Fedha na Uchumi kwa ujumla, kutajenga hadhi ya mwandishi pamoja na kuwa na nafasi nzuri ya kuandika, kuripoti na kutoa elimu kwa jamii.

Makame, ambaye taasisi yake ZRA ni miongoni mwa zilizodhamini mkutano wa nane wa TEF, alisema wanatamani kuona waandishi maalum wakiandika habari za Kodi zitakazoelimisha jamii umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii.

Pia alisema, waandishi wanaweza kuchagua tahsusi wazipendazo, kama vile sekta ya elimu, uchumi wa buluu, afya, mazingira, michezo, kilimo, habari za utalii na nyengine na kuandika kwa weledi na uhakika zaidi.

“Kwa bahati mbaya, nchini kwetu hakuna uandishi uliojikita eneo fulani yaani ‘specialization’. Mwandishi yuko kila eneo na kote huko anaandika habari za matukio za kuzungumzwa na watu badala ya kutafiti, kukusanya taarifa na kuzichambua kitaalamu,” alifafanua.

Alifahamisha kuwa, ili kufikia lengo hilo, wahariri wana nafasi kubwa kuwatengeneza wanahabari wao kwa kuwasomesha na kuwapatia nyenzo na stahiki zao ipasavyo, badala ya kuwaacha wakihangaika na uandishi usiozingatia weledi.

Khamis alisema, ili kuhamasisha uandishi wa aina hiyo, ZRA imekuwa ikiwapa muongozo waandishi kwa kuwashajiisha kuandika habari za kodi zilizotafitiwa na kufanyiwa uchambuzi wa kina.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo, walisema kuwa uandishi wa kitahsusi unapaswa kuanza na mwandishi mwenyewe kwa kuamua kwa dhati kujielekeza kwenye sekta anayotaka na kwamba wahariri wapo tayari kuendeleza uweledi wa muandishi husika pindi akionesha utayari.

About The Author

(Visited 6 times, 1 visits today)

Last modified: November 11, 2024

Close