Visit Sponsor

Written by 8:48 am KITAIFA Views: 18

SAFARI YA MWENGE WA UHURU KUFIKA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO NI REKODI NYINGINE YA SAMIA

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI

MOSHI

Historia inaendelea kuandikwa leo wakati Mwenge wa Uhuru ukianza safari ya kupandishwa hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika, ukiwa na urefu wa mita 5,895.

Hii ni mara ya tatu kwa Mwenge wa Uhuru kufanikisha safari hii, hatua inayolenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuendeleza falsafa ya umoja, amani, na maendeleo.

Sherehe rasmi za kuzimwa kwa Mwenge huo zilifanyika jana jijini Mwanza.

Katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikabidhi Mwenge kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kuendelea na jukumu la kuupeleka kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Kupandishwa kwa Mwenge huu ni sehemu ya mwendelezo wa historia iliyoanzishwa na awamu za serikali zilizopita, ikiwa ni alama ya kuhimiza uzalendo na mshikamano wa kitaifa.


Akizungumza katika eneo la Marangu, lango rasmi la kuanzia safari ya kupanda mlima Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Jully Lyimo, alieleza umuhimu wa tukio hili.

Alisema kuwa safari hii ni heshima kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuendeleza tamaduni na kumbukumbu muhimu za kitaifa.

“Tangu mara ya kwanza Mwenge huu ulipopandishwa mwaka 2011, sasa tunafanya hivyo kwa mara ya tatu, tukitilia mkazo mshikamano na amani,” alisema Lyimo.

TANAPA na JWTZ wamefanya maandalizi kabambe kuhakikisha usalama na mafanikio ya safari hiyo, ikiwahusisha wapandaji wenye uzoefu na kuzingatia hali ya hewa ya mlima.

Hali ya hewa kwenye Mlima Kilimanjaro inaweza kubadilika ghafla, hivyo vikosi vilivyopewa jukumu la kupandisha Mwenge vimepewa mafunzo maalum kuhakikisha wanafanikisha safari hiyo kwa ufanisi na usalama.


Kupandishwa kwa Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro si tukio la kawaida bali lina maana kubwa kwa taifa. Mwenge wa Uhuru, ambao ulianzishwa mara baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, unaakisi ujumbe wa maendeleo, amani, na mshikamano.

Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliufananisha Mwenge huu na mwanga unaoangaza giza, ukiwakilisha matumaini ya taifa jipya huru lililokuwa linaelekea katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa kupandisha Mwenge huu katika kilele cha Afrika, Tanzania inatoa ujumbe kwa dunia nzima kuhusu umuhimu wa mshikamano wa kitaifa na uvumilivu wa wananchi wake.

Aidha, ni fursa ya kipekee kuendeleza utalii wa mlima Kilimanjaro, ambao ni kivutio kikubwa cha watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Lyimo aliongeza kuwa tukio hilo linaenda sambamba na juhudi za TANAPA katika kukuza utalii wa ndani na kuhamasisha Watanzania kuthamini vivutio vyao vya asili.


Safari ya kupandisha Mwenge wa Uhuru hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo mwinuko mkali, baridi kali, na upungufu wa oksijeni.

Hata hivyo, wapandaji walioteuliwa kwa ajili ya safari hii ni wale waliopewa mafunzo maalum na wana uzoefu wa kushinda changamoto hizo.

Timu ya JWTZ imekuwa ikishirikiana na waongoza watalii na watoa huduma wa eneo la Marangu kuhakikisha kila hatua ya safari hiyo inakwenda kwa mpangilio mzuri.

Kwa mujibu wa Kamishna Lyimo, safari hiyo inatarajiwa kuchukua siku tano hadi saba kufikia kilele na kurejea salama. “Huu ni mlima unaohitaji nidhamu ya hali ya juu na maandalizi thabiti.

Tunashukuru timu yetu ya wapandaji ina ari kubwa na imejizatiti kuhakikisha wanapandisha Mwenge huu hadi kileleni,” alisema.


Kupandishwa kwa Mwenge wa Uhuru hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro kunatoa pia nafasi ya kuutangaza mlima huo kimataifa.

Mlima Kilimanjaro ni miongoni mwa Maajabu Saba ya Afrika na umeorodheshwa kama Urithi wa Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO).

Tukio hili linatarajiwa kuvutia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, hivyo kuongeza mwonekano wa Mlima Kilimanjaro na kuvutia watalii zaidi.

Mkuu wa TANAPA, Lyimo, alibainisha kuwa mlima huo unachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya hifadhi na kusaidia maendeleo ya kiuchumi ya jamii zinazozunguka eneo hilo.

“Utalii wa mlima huu ni kichocheo cha maendeleo ya kijamii, na tukio hili litahamasisha Watanzania zaidi kutembelea na kufurahia rasilimali za nchi yao,” alisema.


Salum Chang’a mkazi wa Moshi anasema kuwa Mwenge wa Uhuru unapopandishwa tena kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, unawakilisha safari ya matumaini na mshikamano wa taifa.

Kupitia tukio hili, Tanzania inakumbusha wananchi wake na dunia juu ya umuhimu wa kuendeleza amani na maendeleo ya pamoja.

Aidha, tukio hili linahamasisha uzalendo na linatoa fursa muhimu ya kukuza utalii wa ndani na nje.

Huku Johari Samson wa Marangu anasema kuwa  Kwa mara nyingine, historia inaandikwa kupitia safari hii, ikidumisha kumbukumbu ya umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa maendeleo ya taifa.

Tanzania inapoendelea kusonga mbele katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi, tukio hili linakumbusha umuhimu wa mshikamano wa kitaifa na jitihada za pamoja katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru utabaki kuwa mwanga unaoongoza Watanzania katika safari yao ya kuijenga nchi yenye mafanikio na mshikamano thabiti.

Akizindua Kitabu cha Historia ya Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisisitiza umuhimu wa mwenge huo kwa historia ya Tanzania, na akabainisha kuwa historia ya Mwenge wa Uhuru haiwezi kutenganishwa na historia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Kuna historia kubwa sana katika Taifa letu, na historia hiyo haiwezi kutenganishwa na historia ya Mwalimu Nyerere.

Nina furaha kwamba leo tumezindua rasmi kitabu cha historia na falsafa ya Mwenge wa Uhuru, kinachoelezea misingi na historia ya mwenge huu.

Tunamshukuru Hayati Balozi Job Lusinde kwa kutuachia kumbukumbu hii adhimu, Mwenyezi Mungu amrehemu mzalendo wetu huyu,” alisema Rais Samia.

Akiendelea, Rais Samia aliwapongeza wote waliofanikisha kukamilika kwa kitabu hicho, akisema kuwa kupitia kitabu hicho Watanzania watapata fursa ya kuelewa jinsi Mwenge wa Uhuru ulivyoanzishwa kabla ya Uhuru na mchango wake kwa Taifa katika vipindi mbalimbali vya kihistoria.

“Nawashukuru wote waliowezesha kitabu hiki kukamilika. Kupitia kitabu hiki tunapata kufahamu namna ambavyo Mwenge wa Uhuru ulivyoasisiwa na jinsi ulivyoendelea kuangazia maisha ya Watanzania katika nyakati tofauti za mapito ya Taifa letu,” aliongeza Rais Samia.

Rais Samia pia alibainisha kuwa kitabu hicho kinatoa mwanga juu ya nafasi ya vijana katika mbio za mwenge kama tunu aliyoiacha Mwalimu Nyerere, na kwamba kitabu hicho kinaendelea kuimarisha na kulinda tunu ya Taifa.

Akizungumzia miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru, Rais Samia alisema, “Mwenge wetu wa Uhuru umetimiza miaka 60.

Falsafa hii imeendelea kufanya kazi na kutekeleza dhamira ya kuasisiwa kwake.

Ingawa kuna mabadiliko makubwa duniani, bado Taifa letu linaendelea kushikilia falsafa hiyo kwa kutumia mbinu tofauti zinazoendana na mifumo mipya ya siasa na uchumi duniani.”

Uzinduzi wa kitabu hicho ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru, ambao umekuwa na nafasi kubwa katika kuhamasisha maendeleo, umoja wa kitaifa, na mshikamano tangu kuasisiwa kwake na Mwalimu Julius Nyerere

About The Author

(Visited 18 times, 1 visits today)

Last modified: October 16, 2024

Close