Visit Sponsor

Written by 6:52 am BIASHARA Views: 12

ZRA YAVUNJA REKODI YA MAKUSANYO ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI

* Yakusanya bilioni 76.497/- sawa na asilimia 103.31 ya makusanyo mapato yaliyotarajiwa



ZANZIBAR

MAMLAKA ya Mapato Zanzibar (ZRA), imevunja rekodi ya makusanyo ya kodi kwa Septemba mwaka huu kwa kukusaya kiasi cha Shilingi bilioni 76.497/- sawa na asilimia 103.31.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuvuka lengo kwa mwezi Septemba mwaka huu ZRA ilikadiriwa kukusanya Shilingi bilioni 74.049.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Zanzibar, Kaimu Kamisna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed alisema kuwa hatua hiyo inatokana na kazi kubwa yeye ufanisi iliyofanywa na ZRA.

“Aidha, Makusanyo halisi ya mwezi Septemba ya mwaka uliopita wa 2023/2024, yalikuwa ni Shilingi bilioni 61.694 ambayo yakilinganishwa na makusanyo halisi ya Septemba ya Mwaka huu wa Fedha wa 2024/2025, yanaonesha ukuaji wa Makusanyo halisi wa asilimia 23.99.

“Katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, ZRA ilikadiriwa kukusanya Shilingi bilioni 194.031 na imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 200.934 ambao ni ufanisi wa asilimia 103.56 wa makusanyo ya mapato yaliyotarajiwa.

“Kwa kulinganisha na makusanyo halisi ya robo ya kwanza ya mwaka uliopita wa 2023/2024, yalikuwa ni Shilingi bilioni 161.831 ambayo yakilinganishwa na makusanyo halisi ya robo ya kwanza ya Mwaka huu wa Fedha wa 2024/2025, yanaonesha ukuaji wa makusanyo halisi wa asilimia 24.16 ,” alisema Kamishna Mohamed

Akielezea sababu za kufanya vizuri, Kamishna Mohamed alisema kuwa ufikiaji wa lengo la makusanyo ya kodi kwa asilimia 103.56, pamoja na mambo mengine umesababishwa na kuimarika na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, zinazotokana na sera na uongozi  mzuri wa  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zilizoimarisha mazingira ya biashara kwa pande zote mbili za Muungano.

“Uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi Zanzibar unaotokana na utekelezaji wa sera nzuri za  kiuchumi za Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

“Kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri na walipakodi ikiwemo kusaidia kurahisisha biashara zao (Trade Facilitation) pamoja na kuwafikia na kuwasilikiza walipakodi kupitia njia mbali mbali ikiwemo kuwatembelea na kwa kutumia kituo cha Mawasiliano kwa Walipakodi cha ZRA (ZRA Contact Center) na Programu ya kupokea Maoni ya Funguka (ZRAFunguka App) kulikopelekea kuongezeka kwa ulipaji kodi wa hiari .

“Kuimarika kwa matumizi sahihi ya mifumo katika usimamizi wa kodi ikiwemo matumizi ya mfumo wa risiti za kieletroniki (VFMS) na matumizi ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa ZIDRAS sambamba na kuongezeka kwa utoaji wa elimu ya kodi kupitia njia mbalimbali,” alisema

Aidha, Kamishna Mohamed alitaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa ufuatiliaji wa karibu wa Walipakodi kulikotokana na kuongeza idadi ya watumishi (wa ajira ya muda)  wa Mamlaka kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma Kikodi kwa Walipakodi na jamii kwa ujumla.

“Utekelezaji wa marekebisho ya Sheria za Kodi kwa mwaka wa Fedha 2024/2025. Hatua hii imepelekea kuimarika kwa ukusanyaji katika vianzio vya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ushuru wa bidhaa, ada za Bandari na Kodi ya Miundombinu.

“Kuimarika kwa ushirikiano baina ya Wizara na Taasisi nyingine zinazofanya kazi na ZRA ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kamisheni ya Utalii na taasisi zote za Serikali sambamba na kuimarika kwa Mahusiano na  Ushirikiano kati ya ZRA na Wafanyabiashara kulikopelekea kuongezeka kwa ulipaji kodi wa hiari,” alisema

MIKAKATI YA UKUSANYAJI ROBO YA PILI

Katika kuimarisha Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi  kwa Robo ya pili ya Mwaka wa Fedha wa 2024/2025 (Oktoba – Disemba 2024), alisema ZRA itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali.

“Kuendelea kufanya ziara kwa Walipakodi ili kutambua na kutatua changamoto za wafanyabiashara na migogoro ya kikodi kwa wakati, ikiwemo kuweka mazingira ya usimamizi wa sheria za kodi yatakayondoa changamoto za wafanyabiashara.

“Kushirikiana na Jumuiya za Wafanyabiashara katika kusimamia Walipakodi kuunganisha mifumo yao ya kibiashara na Mfumo wa kutolea risiti za kielektroniki (VFMS) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za Walipakodi.

“Kufanya Kampeni mbali mbali zenye lengo la kuuhamasisha ulipaji wa Kodi wa hiyari katika Mikoa yote. Kampeni zitalenga kuongeza idadi ya Walipakodi kwa kufanya usajili pamoja na kuhamasisha matumizi sahihi ya mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki (VFMS) na elimu ya Kodi kwa ujumla.

“Kufanya tafiti kwa lengo la kupata majibu ya Kisayansi yatakayoongeza urahisi wa kulipa Kodi kwa kuondoa changamoto zinazojitokeza,” alisema Kamishna Mohamed

Pamoja na hali hiyo alisema kuwa wataendelea weledi wa watumishi wa ZRA kwa kuwapatia mafunzo stahiki, usimamizi makini, na huduma nzuri kwa walipakodi (Customer care).

Licha ya hali hiyo alisema mkakati mwingine ikiwamo kuwachukulia hatua za Kisheria Walipakodi wachache wasiowajibika ipasavyo katika kutimiza wajibu wao wa kulipa Kodi.

Alisema Mamlaka ya Mapato Zanzibar inaendelea kuwashukuru Walipakodi wote kwa kuwajibika kwa hiyari katika ulipaji wa Kodi kwa katika kipindi cha miezi mitatu ya Julai – Septemba 2024.

“Uwajibikaji huu wa hiyari ni ishara ya uzalendo katika kutekeleza wajibu wao wa kisheria sambamba na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

“ZRA itaendelea kurahisisha biashara za Walipakodi pamoja na kuimarisha mahusiano mema ili kuleta ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na hatimaye kuiwezesha Serikali kuendelea kuimarisha  huduma bora za kijamii na maendeleo kwa wananchi wote,” alisema Kamishna Mohamed

About The Author

(Visited 12 times, 1 visits today)

Last modified: October 3, 2024

Close