Visit Sponsor

Written by 4:46 am KITAIFA Views: 17

SABABU YA ‘WALIOTUMWA NA AFANDE’ KWENDA JELA MAISHA

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI DODOMA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma, imewahukumu kifungo cha maisha gerezani washtakiwa wanne maarufu ‘waliotumwa na afande’, baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

Ni katika kesi ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 iliyokuwa inawakabili washtakiwa hao akiwamo MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo ambaye ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Hukumu hiyo imetolewa jana Septemba 30, 2024, ambapo pia Mahakama hiyo imewataka kila mmoja kumlipa binti huyo fidia ya Shilingi milioni 1.

Hatua ya hukumu ya kesi ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam ambapo kesi hiyo imekuwa na hisia tofauti miongoni mwa wana jamii.

Ijumaa ya Septemba 27, 2024, wakili wa washtakiwa hao, Meshack Ngamando akizungumza na waandishi wa habari alisema kila kitu kilichotakiwa kwenye kesi hiyo kilikuwa kimekamilika, hivyo kinachosubiriwa ni uamuzi wa Mahakama.

Alisema siku hiyo ya Ijumaa walifanya mawasilisho ya mwisho ya kisheria kuhusu mwenendo mzima wa kesi hiyo na kwamba wamewasilisha hoja kuhusu kasoro zilizojitokeza wakati wa usikilizwaji.

“Tumepata nafasi ya kuwasilisha mawasilisho ya mwisho, kuhusu mwenendo wote wa kesi kuanzia hati ya mashtaka, ukamataji, utambuzi, mashahidi, vielelezo vilivyotolewa mahakamani kwa muda wa saa tatu kuanzia saa nane mchana hadi saa 11.00 jioni.

“Upande wa Jamhuri pia umewasilisha yao kuanzia saa 11.00 jioni hadi saa moja usiku, kwa hiyo kinachosubiriwa kwa sasa ni uamuzi wa Mahakama,”  alisema Ngamando.

About The Author

(Visited 17 times, 1 visits today)

Last modified: October 1, 2024

Close