Visit Sponsor

Written by 8:56 am KITAIFA Views: 28

KAMA UNAKWEPA KODI ‘USIOE’ BABLA

Na Mwandishi Wetu


Wananchi Visiwani Zanzibar wametakiwa kuzingatia suala la kuwajibika katika kulipakodi kabla ya kuziendea ndoa ili kuipa nafasi Serikali nguvu ya kutoa huduma kwa wananchi wake.


Wito huo ulitolewa jana na Mstahiki Meya wa Baraza la Mji Kaskazini “A” Unguja Mheshimiwa Machano Fadhil Machano Babla wakati akifungua Mkutano wa elimu ya Mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa Walipakodi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Akizungumza katika Mkutano huo ulioandaliwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Mstahiki Meya alisema ni lazima kwa kila kijana awajibike katika suala la Kodi kabla hajaingia katika ndoa kwa kuwa kizazi kinachopatikana kinatarajia Kodi zinazokusanywa na Serikali ili kupata huduma bora za Kijamii.


Mheshimiwa Babla alifafanua kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa huduma mbali mbali kwa wananchi wake bila malipo hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kufahamu kuwa Serikali inaweza kugharamia mambo hayo kutokana na Kodi inazokusanya.


Alibainisha kuwa, iwapo Wazanzibari wanahitaji kuwa na Serikali ambayo itaweza kuhudumia vizazi na jamii ya Wazanzibari kwa ujumla, suala la kodi linapaswa kupewa kipaumbele kabla vijana hawajaamua kuingia katika Ndoa.


Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi katika Mkutano huo, Meneja wa Kodi Mkoa wa Kaskazini Unguja ndugu Hanii Mohamed Khamis aliwataka wafanyabiashara kuendelea kutoa mashirikiano kwa ZRA ili kuifanya kazi ya ukusanyaji wa mapato na ulipaji kodi iwe rahisi kwa pande zote mbili.


Aliongeza kuwa, Wafanyabiashara wana wajibu wa kuendelea kufanyabiashara kwa kufuata misingi ya Sheria za kodi ikiwemo kuwasilisha malipo kwa wakati sambamba na kutoa Risiti za Kielektroniki kila wanapofanya mauzo.


Naye Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi kutoka ZRA ndugu Makame Khamis Moh’d wakati akiwasilisha mada katika mkutano huo alisema marekebisho ya Sheria za Kodi pamoja na mambo mengine yamezingatia uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha uwekezaji katika Uchumi wa Buluu.


Miongoni mwa Sheria zinazosimamiwa na ZRA ambazo zimefanyiwa marekebisho kwa mwaka huu ni pamoja na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sheria ya Kodi ya Majengo Pamoja na Sheria ya Ushuru wa Bidhaa.

About The Author

(Visited 28 times, 1 visits today)

Last modified: September 14, 2024

Close