Visit Sponsor

Written by 4:07 pm KITAIFA Views: 44

WAZIRI MKUU AMUAGIZA WAZIRI WA MAJI KUFUATILIA UTENDAJI KAZI RUWASA LINDI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua moja ya mtambo uliotolewa na Serikali kwa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini, (RUWASA) kwa ajili ya kuchimba visima Mkoani humo, alipofanya ziara katika ofisi za Mamlaka hiyo Januari 8, 2024. Tangu kupokelewa kwa mitambo hiyo mwezi wa sita mwaka jana mitambo hiyo haijafanya kazi iliyotarajiwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kufika katika ofisi za wakala wa Maji na usafi Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Lindi (LUWASA) kufuatilia mapungufu yaliyopo ikiwemo kutotumika kwa gari la uchimbaji visima lililotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu Juni, 2023 ili kuwezesha uchimbaji wa visima vya maji. 

“Hii wizara ina Waziri makini sana, mnafanya vitu kwa ufichouficho, sasa Waziri aje hapa, mnamuona anavyohangaika Waziri wenu, vitu vidogo vidogo hivi mpaka waziri aje na ninyi mpo, kwanini mpo hapa,” Waziri Mkuu alisisitiza na kuongeza kuwa anahitaji taarifa ya kwa nini mashine hiyo tangu imefika haijachimba kisima hata kimoja.

Ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Januari 8, 2024, baada ya kufanya ziara katika ofisi za RUWASA zilizopo Manispaa ya Lindi na kushuhudia mtambo wa kuchimba visima ukiwa umeegeshwa na hakuna kisima kilichochimbwa tangu ulipotolewa mwaka jana huku katika mikoa mingine iliyopewa mtambo kama huo visima vinachimbwa kama ilivyokusudiwa.

Waziri Mkuu amehoji “Ni kwanini mtambo huu haujaanza kufanya kazi kwa kipindi cha miezi sita ikiwa katika mikoa mingine imeshaanza kufanya hivyo. Mwezi wa sita hadi leo hamjachimba hata kisima kimoja na mnasema kuna matope haiwezekani. Mheshimiwa Rais ameleta mtambo wananchi wameona gari limefika mnataka visima visichimbwe?”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alihoji sababu ya kutotumika kwa pikipiki zilizonunuliwa na RUWASA Mkoa wa Lindi tangu mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa jumuiya za watumia maji kwa madai kuwa bado hazijapata usajili. “Huu ni uzembe haiwezekani fedha za wananchi zinapotea nyie mpo tu. Hizi pikipiki zimeanza kuharibika.”

Akizungumzia kuhusu pikipiki hizo Afisa Manunuzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) Bw. Kenedy Mbagwa alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia suala la vibali vya kutumia pikipiki hizo kutoka makao Makuu ya RUWASA bila ya mafanikio, ambapo Waziri Mkuu baada ya kupata maelezo hayo amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Lindi afuatilie suala hilo.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amechukizwa na hali ya mazingira ya ofisi ya LUWASA ambayo haiendani na ofisi za umma kwani ni machafu na yana vichaka vingi. “Hapa ndio ofisini, kwa hiyo hapa tupo kazini,” alihoji wakati alipokuwa akikagua maeneo hayo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maji na Msajili wa Hazina wafanye tathmini ya kina kuangalia utendaji kazi wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ambayo ipo ndani ya Ruwasa kuona kama ipo haja ya taasisi hiyo kuendelea kujitegemea. “Hamuwezi kuwa na agency mbili, zinazofanya kazi moja kwenye taasisi moja.”

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA mkoa wa Lindi, Mhandisi Muhibu Lubasa alisema mkoa umejipanga kuanza kuchimba visima katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa kutumia mtambo huo uliotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia mwezi Februari mwaka huu.

About The Author

(Visited 44 times, 1 visits today)

Last modified: January 8, 2024

Close