WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba ameeleza mafanikio yaliyotokana na mikutano na ziara alizofanya hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Waziri Makamba amesema Mikutano na ziara hizo zimeleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa, kubwa ikiwa ni kuimarisha uhusiano wa uwili (bilateral relations), kuendeleza ushirikiano wa sekta za kimkakati na kuimarisha utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Kuhusu ushiriki katika Mikutano ya Jumuiya za Kikanda na Kimataifa akianza na ziara ambayo Rais Dkt. Samia alijifanya Kanda ya Asia katika Nchi ya India Oktoba 2023 amesema ziara hiyo ililenga, kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na India.
“Hususan katika sekta za kimkakati kama afya, viwanda na biashara, ulinzi na usalama, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji na kilimo na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji za Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka India,” amebainisha Waziri Makamba.
Akizungumzia ma Mafanikio yaliyopatikana kutokana na ziara hiyo amebainisha kuwa ni pamoja na kupatikana kwa soko la tani 200,000 za mbaazi kwa kila mwaka, na uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya India hapa nchini.
Nyingine ni kufanyika kwa kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India lililoazimia kuongeza soko la bidhaa za kilimo kutoka Tanzania kwenda nchini India na kuongeza uhakika wa soko hilo, kuweka quota ya kutosha katika mazao muhimu kama mbaazi, kuongeza muda ambao kampuni za India zinaruhusiwa na Benki Kuu ya India kutoa bidhaa kwa mkopo kwa kampuni za Tanzania (Credit Line Time Limit) kutoka siku 180 mpaka 360; sekta binafsi kukubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta za kilimo, teknolojia, sanaa na burudani, uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi wa nchi zote mbili.
Kadhalika Kampuni kubwa za India zinazojishughulisha na sekta za afya, kilimo, usafirishaji, maji, nishati, zikiwemo kampuni za TATA, Hospitali ya Apollo, Bharti Enterprises, Bajaj Wapcos zilionesha nia ya kuwekeza hapa nchini.
Waziri Makamba amesema pia, hivi karibuni, tumeshuhudia Kampuni ya Mahindra ya India ikiwekeza nchini uanzishwaji wa kiwanda cha kupanga magari (assembling facility for cars) chenye thamani ya bilioni 10.
Kwa upande ziara ya Kikazi ya Rais Dkt. Samia aliyoifanya jijini Davos, Uswisi mwezi Januari 2023, amesema Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum-WEF) lililofanyika mwezi Januari 2023 Davos, Uswisi.
Hivyo Rais Dkt. Samia aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa hilo ambapo akiwa nchini Uswisi, Mheshimiwa Rais alishiriki mikutano iliyoandaliwa na WEF, mikutano ya pembezoni, pamoja na mikutano ya uwili.
Kwamba Mafanikio yaliyopatikana katika ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo ni pamoja na Tanzania kutengewa Dola za Marekani milioni 550 ili kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika na kuandaa Mpango wa Miaka Mitano (2023 – 2027).
Aidha, Tanzania ilipata nafasi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Mapinduzi ya Kilimo Afrika (AGRF) la Africa Food Systems Forum 2023 uliofanyika nchini mwezi Septemba 2023.
Vile vile WEF iliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufanya Tanzania kuwe moja ya Eneo la Mapinduzi ya NNE ya Viwanda Duniani (4th Industrial Revolution Hubs) yatakayoanzishwa kwenye nchi 20 duniani;
Kadhalika baadhi ya wawekezaji na kampuni zilizoshiriki mkutano huo zimeanza hatua za awali kuwekeza Tanzania, vile vile, baadhi ya Kampuni kama vile Engro Corp kutoka nchini Pakistan zilionesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea ya kukuzia (Urea); Shirika la Icea Lion, ambalo lina nia ya kufanya mradi wa miti ya mikoko wanaoutekeleza ili kupunguza athari za hewa ya ukaa;
Kwamba kupitia mazungumzo kati ya Mheshimiwa Rais, Bw. Schwan, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Roche AG alielezea utayari wa kampuni yake kuwekeza Tanzania katika tafiti za dawa, na Kansela wa Ujerumani alionesha utayari wa nchi yake kuwekeza katika gesi asilia;
Waziri Makamba ameeleza, WEF walikubali ombi la Tanzania kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Uchumi la Kanda pale mikutano hiyo itakapoanza tena; ii. Jukwaa la Uwekezaji Afrika lililofanyika mjini Marrakesh, Morocco.
About The Author
Last modified: December 18, 2023