Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais-
UTUMISHI ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS,
PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli
amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Utumishi wa Umma kwa
kuhimiza uwajibikaji wa hiari wa mtumishi kwa kujaza kazi anazofanya
kila siku katika mfumo mahali popote ili kuongeza tija katika utoaji wa
huduma kwa umma.
Ameyasema hayo leo tarehe 12 Desemba, 2023 wakati wa kufungua
mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi
wa Umma na Taasisi (PEPMIS na PIPMIS) na Mfumo Maalum wa
Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini (HR Assesment) kwa
viongozi na watumishi wa Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Hazina
Jijini Dodoma.
Bi. Felista amefafanua kuwa mfumo wa PEPMIS utawezesha viongozi
kusimamia utendaji kazi wa watumishi bila upendeleo na utaongeza
ufanisi, PIPMIS itawezesha kupima utendaji kazi wa Taasisi za Umma
na HR Assesment itawezesha kufanya Tathmini ya hali ya
Rasilimaliwatu Serikalini na kuitumia ipasavyo.
Aidha, Bi. Shuli ameongeza kuwa hali ya mafunzo kwa Mkoa wa
Dodoma inaendelea vizuri na anaamini yatakamilika kama ilivyopangwa
kwa kuwa pande zote zinazohusika na mafunzo zinatoa ushirikiano
mkubwa kwa wakati.
“Wawezeshaji wote wako vizuri na watumishi kutoka katika Wizara na
Taasisi zote wanaitikia wito na wanakuja na kompyuta ambazo ni
kitendea kazi muhimu sana katika mafunzo haya” amesema Bi.Felista.
Vilevile, amesema mfumo wa PEPMIS umekuja kuwa mbadala wa
OPRAS ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan anayelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji inayowezesha
viongozi na watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao
kwa ufanisi wakati na mahali popote.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa
Rasilimaliwatu wa Wizara ya Fedha Bw. Renatus Msagira amesema
watumishi wako tayari kujifunza na kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi kwa
maendeleo ya taifa.
“Tuko tayari na hatutakuwa kikwazo katika utekelezaji wa jitihada hizi
muhimu za Serikali ambazo lengo lake ni kuhakikisha wananchi
wanapata huduma bora kwa wakati” amesisitiza Bw. Msagira.
Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment yanaendeshwa na Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika
Mikoa yote Tanzania Bara na yatahitimishwa Desemba 31,2023.
About The Author
Last modified: December 13, 2023