Visit Sponsor

Written by 1:48 pm KITAIFA Views: 29

SERIKALI KUCHUKUA HATUA KWA WALIOMZUSHIA KIFO MAKAMU WA RAIS

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye,
ametangaza nia ya serikali kuchukua hatua za waliomzushia kifo Makamu wa Rais
Dkt. Phillip Mpango, ili kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao na kuwalinda
wananchi dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao.
Kupitia mtandao wake wa kijamii wa X tarehe 10 Disemba 2023, Waziri Nape
Nnauye alisisitiza kwamba serikali ina sheria zinazoelekeza matumizi sahihi ya
mtandao pamoja na taasisi na watu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo ili
kulinda watumiaji mitandao na wananchi kwa ujumla.

Aidha, Waziri amehakikishia umma kwamba hatua zitachukuliwa kwa kuzingatia
sheria hizo bila kuathiri uhuru wa watu, akionyesha matumaini kwamba wananchi
wataelewa nia njema ya serikali katika kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao.
Maoni yake yamepokelewa kwa namna tofauti na umma, huku baadhi wakitoa maoni
yao kuhusu hatua hizo za udhibiti wa matumizi ya mtandao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa simu, Waziri Nape alisema kuwa
matumizi salama ya mtandao ni muhimu sana katika kuhakikisha amani na usalama
wa nchi unakuwepo. Amesema zipo sababu za msingi na umuhimu wa matumizi
salama ya mtandao kwa kuepuka matumizi mabaya kama ilivyotokea hivi karibuni
kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kumzushia kifo Mhe. Makamu wa
Rais.


Akifafanua umuhimu wa kukuza amani na utulivu kwa nchi amesema “matumizi
mabaya ya mtandao yanaweza kusababisha taharuki na hata kuhatarisha amani na
utulivu wa nchi. Kutoa taarifa za uzushi wa kifo kwa wananchi kunaweza kuchochea
hofu na wasiwasi kwa jamii.”
Amesema pia kuwa kulinda heshima za wananchi wote, matumizi mabaya ya
mtandao yanaweza kudhuru sana heshima na hadhi ya wananchi kwa ujumla.

Amefafanua kuwa kutoa taarifa na kuzusha kuhusu kifo kwa mtu yeyote ni ukiukwaji
wa heshima na utu wa mtu na inaweza kuathiri maisha yao na kuleta mtafaruku usio
na sababu.

“Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanaweza kutumiwa kwa urahisi
kutengeneza na kusambaza habari potofu na za uongo. Kumzushia mtu kifo ni
mojawapo ya mbinu zinazoweza kutumika kudanganya umma na kusababisha
machafuko. Tunalazimika kama Serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
wanaovunja sheria za matumizi salama ya mtandao. Kwa kufanya hivyo, tunaweza
kujenga jamii inayoheshimu mawasiliano na inayofanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya
maendeleo na amani ya nchi.” ameongeza Mhe. Waziri Nape Nnauye.


Mhe. Nape amesisitiza umuhimu wa kuwaheshimu na kulinda usalama wa viongozi
na wananchi kwa kuhakikisha watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaheshimu
maadili na kanuni pamoja na sheria za matumizi ya mawasiliano ikiwemo mitandao
ya kijamii. “Matumizi mabaya ya mtandao yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa
wananchi. Kutoa taarifa za uongo za kifo cha mtu, kunaweza kusababisha taharuki
kwa familia, ndugu na jamaa zake na wananchi kwa ujumla, hivyo ni muhimu
kuchukua hatua za kuzuia matendo kama haya” amesema Mhe. Nape.


Mhe. Nape pia amesisitiza umuhimu wa Serikali kuweka mazingira salama ya
mawasiliano nchini ili kuhakikisha matumizi salama ya mtandao. “Tunaweza kujenga
mazingira salama ya mawasiliano ambayo yanawawezesha wananchi kutoa maoni
yao kwa uhuru bila kutumia njia za uongo na chuki kwa nia ya kudhalilisha na kuleta
taharuki kwa jamii” amesema Mhe. Nape.


Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na taarifa kuhusu hali ya afya ya Mhe.
Makamu wa Rais na kuleta mtafaruku mkubwa na hofu kwa wananchi na kwa familia
yake. Serikali imekuwa ikiwakumbusha wananchi umuhimu matumizi salama ya
mitandao kwa maendeleo badala ya kutumia vibaya. Wizara ya Habari, Mawasiliano
na Teknolojia ya Habari imekuwa ikitoa elimu kwa umma umuhimu wa matumizi
salama, ikiwemo mwezi Oktoba 2023 ikiwa ni mwezi wa elimu kwa umma duniani
kuhusu usalama wa matumizi ya mtandao.

About The Author

(Visited 29 times, 1 visits today)

Last modified: December 11, 2023

Close