Visit Sponsor

Written by 10:17 am KITAIFA Views: 57

SIMBACHAWENE AIELEKEZA TASAF KUOKOA MAISHA YAMAMA NA MTOTO KATIKA KIJIJI CHA BUNGU-KOROGWE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Bungu, Kata ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameuelekeza uongozi wa
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufanya tathmini ya ujenzi wa
jengo la afya ya mama na mtoto katika Kijiji cha Bungu, Kata ya Bungu,
Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ili kuwaondolea adha
ya upatikanaji wa huduma hiyo wakazi wa Kata hiyo.
Mhe. Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya
kukagua utekelezaji wa maendeleo ya miradi ya TASAF katika
Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
“Nimesikia katika maelezo yenu kuwa mna changamoto ya upatikanaji
wa huduma za afya hususan ya mama na mtoto, nawaelekeza viongozi
wa TASAF mfanye tathmini ya ujenzi wa jengo la huduma ya mama na
mtoto ambalo litajumuisha huduma zote anazotakiwa kupata mama na
mtoto,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya kazi usiku na mchana kutafuta
fedha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wake na hii ndio zawadi yake
kubwa kwa wananchi, hivyo ni lazima wapatiwe huduma muhimu
ikiwemo hiyo ya jengo la afya.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewapongeza walengwa wa TASAF wa
Kijiji hicho cha Bungu kwa kutumia vizuri ruzuku wanayoipata katika
kufanya mambo ya maendeleo.
“Nimefurahi sana kwa shuhuda mlizozitoa hapa, inaonyesha ni jinsi gani
mnavyotumia vizuri ruzuku ya TASAF mnayoipata, nina uhakika jambo
hili hata Rais wetu mpendwa akilisikia litamfurahisha sana na kuwa na
moyo wa kuendelea kutafuta fedha nyingine ili muendelee kunufaika,”
Mhe. Simbachawene amesisitiza na kuwahimiza walengwa hao
kuendelea kujishughulisha na masuala ya maendeleo ili wasirudi tena
katika umasikini.

2

Vilevile Mhe. Simbachawene amewasisitiza walengwa hao pamoja na
wananchi wa Kijiji cha Bungu kutunza miradi yote iliyoanzishwa katika
kijiji hicho.
“Nimeshuhudia kisima cha maji na nimekunywa maji yake ambayo ni
mazuri, rai yangu kwenu ni kukitunza ili kiwasaidie kwani ni suluhisho
kubwa katika changamoto ya upatikananji wa maji,” Mhe.
Simbachawene amesisitiza.
Mhe. Simbachawene ameendelea na ziara yake ya kikazi ya
kuzungumza na watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi
ya TASAF mkoani Tanga ambapo leo ametembelea Halmashauri ya
Wilaya ya Korogwe.

About The Author

(Visited 57 times, 1 visits today)

Last modified: October 19, 2023

Close