Visit Sponsor

Written by 11:07 am KITAIFA Views: 25

GEITA WAISHUKURU TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE KUWAFIKISHIA HUDUMA YA MATIBABU

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayetoa huduma
katika kliniki maalum ya VIP Grace Mbanga akimpima sukari kwenye damu mkazi
wa Geita aliyetembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa
maonesho ya sita ya kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja
vya EPZA Bombambili mkoani Geita.

Wananchi wa Mkoa wa Geita wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) kwa kufikisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
kwa wananchi hao bila gharama.
Shukrani hizo zimetolewa na wananchi mbalimbali waliotembelea banda la JKCI
lililopo katika maonesho ya sita ya kitaifa ya Teknolojia ya madini yanayoendelea
katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Donard Francis alisema Taasisi ya JKCI
imeonyesha kuwajali watanzania ambao hawakuwa na matarajio ya kuchunguza
mioyo yao kutokana na mazingira waliyopo hivyo kuwaomba kuendelea kushiriki
katika matukio mbalimbali yatakayowapa nafasi wananchi kujua afya ya mioyo
yao.
“Leo kwa mara ya kwanza nimepima moyo wangu, nimepima sukari kwenye damu
na shinikizo la damu, kwakweli sikujua kama kuna umuhimu wa kuchunguza
magonjwa haya hapo awali lakini kupitia Taasisi hii nimepata elimu ambayo
nitawaelimisha na wenzangu umuhimu wa kuchunguza afya zao”, alisema Donard
Kwa upande wake Sada Hassan mkazi wa Geita aliyepatiwa huduma katika banda
la JKCI alisema kuwa yeye ni mjamzito anayetarajia kujifungua wakati wowote
wiki hii lakini tangu alipobeba ujauzito huo hakuwahi kupima shinikizo la damu
hadi wiki hii ya mwisho alipoenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita na
kupimwa shinikizo la damu ambapo majibu yake hayakuwa mazuri.
“Nimetoka kijiji cha Nyang’wale ambapo nimekuwa nikienda kliniki lakini sikuwahi
kupimwa shinikizo la damu, leo nimefika katika banda la JKCI nimepimwa shinikizo
la damu na kuanzishiwa dawa ili niweze kutoka katika hatari ya kupata madhara
wakati wa kujifungua maana shinikizo langu la damu lipo juu”, alisema Sada
Sada alisema amefurahia huduma alizopata katika banda la JKCI kwani hata mtoto
wake aliyopo tumboni ameweza kufanyiwa uchunguzi wa moyo wake na
kuonyesha kuwa yupo salama.

“Wanawake wenzangu ambao wana ujauzito wafike katika banda la JKCI
kuchunguza kama afya zao zipo sawa kuondokana na athari zinazoweza kujitokeza
kipindi cha ujauzito na wakati wa kujifungua kama wataalamu wa afya
wanavyoelimisha”, alisema Sada
Akitoa wito kwa Taasisi nyingine zinazotoa huduma za afya Victor Maduhu
ameziomba Taasisi za afya kuwafuata wananchi walipo kama ambavyo JKCI
imefanya ili wananchi wapate huduma za afya kiurahisi kwani watu wengi
wanahitaji huduma za kibingwa lakini kutokana na hali zao kiuchumi wanakosa
fursa ya kupata huduma hizo.
Victor alisema Serikali imewekeza vizuri katika sekta ya afya ambapo sasa hivi
hakuna haja ya mtu kufuata huduma za kibingwa nje ya nchi kwani huduma zote
za kibingwa zinapatikana hapa Tanzania.
“Naipongeza sana Serikali yangu kuwekeza katika huduma za afya, ila nawaomba
wataalamu wa afya kutoka Taasisi za kibingwa kuiga mfano wa JKCI kutufikia
kwani sisi wananchi wenye uchumi wa chini tunawahitaji sana ili tupate huduma
kwa karibu na kirahisi bila ya kuhangaika”, alisema Victor

About The Author

(Visited 25 times, 1 visits today)

Last modified: September 30, 2023

Close