Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatebwa ( wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Kamati ya Ulinzi na Usalma Mkoa wa Pwani.
Kamati za Usimamizi wa Maafa nchini zimetakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatebwa wakati akifungua Kikao Kazi cha Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na madhara ya El Nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa Mkoa wa Pwani ambapo amesema matukio ya maafa yanatokea na kusababisha madhara katika ngazi ya jamii ambapo Serikali za Mitaa, kuanzia Kitongoji, Mtaa au Kijiji na Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya zinawajibika kuhakikisha usalama wa watu kulinda mali za wananchi.
Amesema kila mmoja anawajibika kuchukua hatua katika eneo lake, akisema mfumo wa Serikali umezingatia wajibu wa sekta na taasisi yenye jukumu kisera na kisheria kuchukua hatua ili kuokoa maisha na mali za jamii kutokana na matukio ya maafa.
“Kikao kazi cha leo kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa. Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea,”Amesema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Hata hivyo amezitaka taasisi zinazohusika kujiandaa kikamilifu kwa kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa dharura wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharura ili ziweze kuchukua hatua kwa haraka na ufanisi kuokoa maisha huku akisema taasisi hizo ni pamoja na zinazohusika na huduma ya utafutaji na maokozi, usalama wa wananchi, afya na makazi ya muda na huduma zingine za kijamii.
“Nazikumbusha taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi pamoja na kuimarisha mifumo kama vile usafiri, mawasiliano, nishati na maji kujiimarisha ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa. Taasisi saidizi zina wajibu wa kuwezesha taasisi zenye jukumu ongozi katika kuokoa maisha na mali ili zitekeleze majukumu kwa ufanisi pamoja na kupunguza athari kwa jamii,” Ameeleza.
Aidha amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua kuzuia madhara kufuatia utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2023 kuonesha uwepo wa El-Niño itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa kwa mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023 na kuendelea mpaka Mwezi Januari 2024.
“Historia inaonesha madhara yanayoweza kutokea katika sekta kutokana na uwepo wa El Nino utakaosababisha mvua kubwa ni pamoja na uharibifu wa miundo mbinu mbalimbali, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali. Maporomoko ya ardhi kuathiri makazi, mazingira, mashamba, usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini,”Amebainisha Bw. Mutatebwa.
About The Author
Last modified: September 29, 2023