Visit Sponsor

Written by 1:57 pm KITAIFA Views: 27

RC CHALAMILA AWATAKA WAFANYABIASHARA KUHESHIMU SHERIA ZA ULIPAJI KODI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara kuheshimu sheria za ulipaji kodi kwa kutoa risiti  na kulipa kodi pindi wanapouza bidhaa zao kwa kutumia mashine za risiti za kielektroniki (EFD).

Pia amewaonya wafanyabiashara kuepuka migomo wakati  wanapofanyiwa mabadiliko ya makadilio  ambayo hawaridhiki nayo, ni vyema wakafika kwenye mamlaka husika ili kutatua changamoto zao.

Chalamila alisema hayo jana wakati akizindua wiki ya mashine za risiti za kielektroniki (EFD) kuanzia Septemba 23 hadi 30 mwaka huu, katika Viwanja  vya Jakaya Kikwete, Dar es salaam.

“Najua chombo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hakiwezi kupendwa msipoteze muda kwenye kupendwa kwasababu Taifa hili linahitaji kodi na kodi ndio mfumo wa Taifa letu kwenda mbele, achaneni na migomo, migomo si afya ni vizuri mkalilia mabadiliko ya sheria na mifumo ya kodi iboreshwe kuliko kuandamana,” alisema Chalamila.

Pia aliitaka TRA iendelee kutoa elimu ya kwa walipa kodi ili kuepusha Migomo isiyokuwa ya lazima.

Kwa upande wa  Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Dinah Edward akimwakilisha Kamisha Mkuu, Alphayo Kidata alisema mkoa wa kikodi wa Ilala ndio unaongoza kwa ukusanyaji wa mapato Tanzania.

“Mkoa wa kikodi wa Ilala ni mkoa mkubwa na unaongoza  kwa makusanyo ya mapato kwa mkoa wa Dar es salaam lakini vilelevile kwa nchi nzima kwa ujumla”.  

Alisema wameendelea kutoa elimu ya kodi pamoja na kujenga vituo vya ukusanyaji kodi kwenye maeneo yaliyokuwa na wafanyabiashara, pia aliitaja mikoa mingine ya kikodi Dar es salaam ambayo ni mkoa wa Temeke na Kinondoni.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiasha wa Kariakoo, Martin Mbwana aliwaahidi viongozi wa Mkoa wa Dar es Salam kuwa wataenda kushirikiana na TRA katika kuhakikisha wanatoa na kudai risiti wakati wakiuza na kununua bidhaa ili kuchangia  maendeleo ya Taifa.

Aidha Mwakilishi wa kampuni ya uuzaji wa mashine za EFD na mashine za risiti za vituo vya uuzaji wa mafuta nchini Radix, Dorah Lusingu alisema katika kutambua umuhimu wa ulipaji kodi wataendelea kuwahimiza wafanyabiashara kutumia mashine za EFD.

“Wafanyabiashara msiogope kutumia mashine za EFD kwasababu zinasaidia ulinzi wa biashara yako pia hata kujua mapato yako unayoyaingiza mwisho wa mwenzi na wa mwaka, pia zinasaidia kutunza kumbukumbu za biashara yako, kujua biashara yako inaendaje pamoja na kujenga uchumi wa taifa letu,” alisema Dorah Lusingu.

Wiki ya mashine za risiti za kielektroniki (EFD), imeanzishwa na TRA kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya mashine za kutoa risiti na kujenga mahusiano kati yake na wafanyabiashara sambamba na utoaji wa elimu ya kodi kwa wananchi na wafanyabiashara katika mikoa ya kikodi ya Ilala, Kinondoni na Temeke.

About The Author

(Visited 27 times, 1 visits today)

Last modified: September 23, 2023

Close