Visit Sponsor

Written by 12:13 pm KITAIFA Views: 24

MAKAMU WA RAIS KATIKA MKUTANO WA UWEKEZAJI SEKTA YA MAJI BARANI AAFRIKA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amesema ushirikiano unahitajika baina ya serikali, sekta binafsi,
wadau wa maendeleo, taasisi za fedha za ndani, azaki pamoja na taasisi za
elimu na utafiti ili kuitekeleza vema kampeni ya uwekezaji katika sekta ya maji
barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema hayo alipomwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika Mkutano wa uzinduzi wa Kampeni ya Jopo la Viongozi wa Juu
kuhusu Programu ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji Barani Afrika uliyofanyika
kando ya Mkutano wa Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa Jijini New York
nchini Marekani. Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana na
Tanzania katika kukusanya rasilimali fedha ili kukamilisha uwekezaji katika
sekta ya maji kwa kuzingatia tayari Tanzania imedhamiria kukusanya takribani
asilimia 43 ya rasilimali fedha kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ili
kufanikisha uwekezaji huo.
Makamu wa Rais amesema Tanzania kama moja ya watekelezaji wa programu
hiyo imeandaa programu ya uwekezaji katika sekta ya maji (TanWIP) ambayo
inatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2024 – 2030. Ametaja malengo ya
uwekezaji huo ni pamoja na kuhakikisha usalama wa maji wa Taifa, uhimilivu
katika athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na upatikanaji wa maji ya
kutosha.
Makamu wa Rais amesema kampeni ya uwekezaji katika sekta ya maji
ilioyozinduliwa Jijini New York itasaidia kukusanya rasilimali zinazohitajika zaidi
kwaajili ya utekelezaji wa programu ya uwekezaji katika sekta ya maji Barani
Afrika. Amesema uwekezaji katika sekta ya maji utahitaji kuongezwa ili kufikia
sehemu ya malengo ya maendeleo endelevu inayohusiana na maji safi na
salama.
Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti Mwenza wa jopo la viongozi wa juu
wa programu ya uwekezaji katika sekta ya maji barani Afrika Rais wa Senegal
Macky Sally pamoja na Mwenyekiti Mwenza mbadala wa jopo hilo Rais
Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Kampeni
hiyo imezinduliwa kwa lengo la kukusanya dola za marekani bilioni 30 ikiwa na
kauli mbiu isemayo “Mind the gap – Invest in Water”

About The Author

(Visited 24 times, 1 visits today)

Last modified: September 21, 2023

Close