UTANGULIZI
Shukrani
- Mheshimiwa Spika, leo tunapoelekea kuhitimisha shughuli za Mkutano wa 12 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukamilisha shughuli za mkutano huu kama zilivyopangwa. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu azidi kutukirimia hekima na nguvu katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku ili tuweze kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
- Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia, kukushukuru wewe binafsi kwa kuendelea kuliongoza vema Bunge hili Tukufu hususan Mkutano huu wa 12 tutakaouhitimisha hivi punde. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Spika amendeelea kuliongoza Bunge hili kwa busara na weledi wa hali ya juu. Hongera sana!
- Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.), Naibu Spika kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukusaidia wewe Mheshimwa Spika kutekeleza majukumu ya kuliongoza Bunge. Vilevile, niwashukuru Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge ambao ni Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb.), Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.) na Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb.) ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi.
- Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango, maoni na ushauri wakati wa mijadala na hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa Mkutano huu. Michango yenu ni muhimu sana kwani imekuwa ikisaidia Serikali katika utekelezaji wa mipango yake hususan katika kutoa huduma kwa wananchi. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inathamini michango yenu, imeipokea na itaifanyia kazi.
Salamu za Pongezi
- Mheshimiwa Spika, kama mtakumbuka katika hatua nyingine ya kuimarisha utendaji ndani ya Serikali, tarehe 30 Agosti, 2023 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaziri. Kutokana na mabadiliko hayo, kipekee nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb.), kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu anayeshughulikia Uratibu wa Shughuli za Serikali na Waziri wa Nishati. Hongera sana na kwa mara nyingine kwa niaba ya watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunakukaribisha na tuko tayari kukupa ushirikiano unaohitajika ili uweze kutekeleza majukumu yako.
- Mheshimiwa Spika, pia, ninawapongeza Mheshimiwa Jerry William Silaa (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mheshimiwa Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi; Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Madini.
- Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza Naibu Mawaziri walioteuliwa, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi; Mheshimiwa Godfrey Msongwe Kasekenya (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi; Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi; Mheshimiwa Judith Savio Kapinga (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
- Mheshimiwa Spika, licha ya teuzi za Naibu Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri. Mheshimiwa Rais alifanya mabadiliko ya baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri pamoja na kufanya uteuzi wa Makatibu Wakuu, Waheshimiwa Majaji na Mabalozi. Nitumie fursa hii kuwapongeza viongozi wote walioteuliwa kushika nyadhifa hizo na kuwatakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yao mapya.
- Mheshimiwa Spika, niwatake viongozi wote walioteuliwa kuzingatia malekezo yote yanayotolewa na viongozi wetu, kufanya kazi kwa weledi, kuimarisha uhusiano mwema, uzalendo na kutanguliza kwanza maslahi ya Taifa letu. Kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyosisitiza, kila mmoja akakiishi kiapo chake na kujituma katika dhamana aliyopewa ili kuleta mabadiliko tarajiwa. Vilevile, zingatieni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026), sheria, sera, kanuni na miongozo mbalimbali ya Serikali.
Salamu za Pole
- Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 1 Julai 2023, Bunge lako Tukufu lilipata pigo la kuondokewa na Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Francis Leonard Mtega aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mbarali, Mkoani Mbeya. Nitumie fursa hii kutoa salamu za pole kwako wewe Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzetu. Hakika atakumbukwa kwa busara zake na mchango wake katika mijadala ya hoja mbalimbali zilizowasilishwa hapa Bungeni. Pia, ninatoa pole kwa Wana CCM wote, wanafamilia, ndugu jamaa marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wetu na tuendelee kumuombea Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa mani na kumpa raha ya milele.
- Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapa pole Watanzania wenzetu wote waliopatwa na majanga mbalimbali yaliyosababisha majeruhi, uharibifu wa mali na kuondokewa na wapendwa wao. Kwa wale majeruhi, tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuimarisha afya zao ili waweze kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.
SHUGHULI ZA BUNGE
Maswali na Majibu
- Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa Bunge, jumla ya maswali 121 ya msingi na mengine ….. ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Pia, jumla ya maswali 7 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yalijibiwa. Niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuweza kujikita katika masuala mahsusi yanayowahusu wananchi na maendeleo ya nchi yetu kupitia maswali mliyoyauliuza.
Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge
- Mheshimiwa Spika, kupitia mkutano huu, Bunge lako tukufu lilipokea na kujadili taarifa moja ambayo ni Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni katika Mkutano wa 10 na Mkutano wa 11 wa Bunge pamoja na utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo mbalimbali katika kipindi hicho.
- Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ilifanyia kazi taarifa ya kuhusu changamoto za utekelezaji wa mkataba wa mauziano ya matrekta ya Kampuni ya URSUS kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na wakulima. Kutokana na taarifa hiyo, kupitia Bunge lako tukufu, ulitoa maelekezo kwa Serikali kufanyia kazi taarifa husika. Nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itayafanyia kazi maelekezo yote kikamilifu.
Miswada ya Sheria
- Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako tukufu limepokea miswada mitatu ya Sheria kama ifuatavyo:-
Moja: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2023 [The Written Laws (Miscellneous Amendment) (No. 2) Bill, 2023]. Muswada ulisomwa katika hatua zake zote;
Mbili: Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2023. Muswada ulisomwa katika hatua zake zote;
Tatu: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2023 (The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.3) Bill, 2023. Muswada huu uliwasilishwa kwa hati ya dharura.
Maazimio ya Bunge
- Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 61 na 107 hadi 112 za Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023, na kwa kuzingatia wajibu wa Bunge, Bunge lako tukufu lilipokea, kujadili na kupitisha maazimio mawili kama ifuatavyo:
Moja: Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009 (The Constitution of the African Civil Aviation Commission, 2009);
Mbili: Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012 (SADC Protocol on Trade in Services, 2012).
- Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kupokea, kujadili na hatimaye kuyapitisha maazimio hayo. Weledi huu wa Waheshimiwa Wabunge unadhihirisha namna Bunge lako Tukufu lilivyosheheni wabobezi wa masuala mbalimbali yanayokusudia kupeleka mbele maendeleo ya nchi na watu wetu.
KILIMO
Mwelekeo wa Mvua za Vuli za Msimu wa Kilimo 2023/2024
- Mheshimiwa Spika, sote tutakumbuka kuwa tarehe 24 Agosti, 2023 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ilitoa utabiri kuhusu mwelekeo wa mvua za vuli kwa mwaka 2023. Utabiri huo unaonesha uwezekano wa kunyesha mvua kubwa kuanzia Oktoba, 2023 ambapo mvua hizo zitanyesha kwa kiwango cha wastani na juu ya wastani katika baadhi ya maeneo. Maeneo yanayotarajia kuwa na mvua hizo ni pamoja na Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kigoma. Mikoa mingine ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Dar es salaam, Pwani na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.
- Mheshimiwa Spika, kiwango hicho cha mvua kitawezesha uzalishaji wa kuridhisha wa mazao ya chakula. Hata hivyo, kuna uwezekano wa mvua hizo kuleta athari katika baadhi ya maeneo kama vile mafuriko yanayoweza kusababisha kutokea kwa mmomonyoko wa udongo pamoja na uharibifu wa miundombinu ya uzalishaji wa mazao.
- Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha mvua hizo zinatumika vizuri na zinaleta tija katika uzalishaji, wakulima wanashauriwa kuzingatia yafuatayo:-
Moja: Kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo kwa wakati ili kuongeza uzalishaji;
Mbili: Kufuatilia kwa ukaribu taarifa za mara kwa mara kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini; na
Tatu: Kuwasiliana kwa ukaribu na kufuata ushauri wa Maafisa Ugani walioko katika maeneo yao;
Upatikanaji wa pembejeo
- Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa pembejeo nchini ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.Sote tunafahamu kuwatija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo hutegemea teknolojia za kilimo, utaalam na upatikanaji wa pembejeo bora ikiwemo mbolea.
- Mheshimiwa Spika, katika msimu wa kilimo 2022/2023, matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 363,599 hadi tani 538,000 sawa na ongezeko la asilimia 48. Ongezeko hili limetokana na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku ambayo Serikali imekuwa ikitoa kuanzia msimu wa kilimo wa 2022/2023. Kipekee, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa mbolea nchini unaimarika.
- Mheshimiwa Spika, ongezeko la matumizi ya mbolea limeenda sambamba na ongezeko la uzalishaji hususan mazao ya chakula ambapo upatikanaji wa chakula umeongezeka nchini.
- Mheshimiwa Spika, makadirio ya mahitaji ya mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024 ni tani 849,219. Hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2023, upatikanaji wa mbolea umefikia tani 480,662 sawa na asilimia 56.6 ya wastani wa mahitaji kwa mwaka. Katika msimu huu wa kilimo, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia makali ya bei ya pembejeo hii muhimu katika uzalishaji. Hivyo, ninaielekeza Wizara ya Kilimo kusimamia kikamilifu ugawaji wa mbolea kwa wakulima kwa kuboresha mfumo wa ugawaji ikiwemo kuongeza vituo vya mauzo ya mbolea pamoja na kuvisogeza vituo hivyo karibu na wananchi.
Hali ya Masoko ya Mazao yaliyovunwa msimu 2022/2023
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa mazao yaliyovunwa katika msimu wa mwaka 2022/2023 yanapata soko la uhakika, bei nzuri na nchi kuwa na uhakika wa usalama wa chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imepanga kununua tani 305,000 za nafaka. Hadi kufikia tarehe 05 Septemba, 2023, jumla ya tani 175,000 za nafaka sawa na asilimia 57 za lengo zimeshanunuliwa kupitia katika vituo 75 vilivyopo katika kanda nane za NFRA. Nitumie fursa hii kuielekeza Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kuimarisha miundombinu ya uhifadhi ili kuepuka kupoteza mazao ya chakula wanayoendelea kununua.
- Mheshimiwa Spika, katika msimu 2022/2023bei za mazao mengine ya biashara zimeendelea kuimarika hususan mazao yanayotumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Mathalan, zao la kakao linalolimwa kwa wingi Wilaya za Kyela na Mvomero bei imefikia shilingi 8,700 kwa kilo. Kwa upande wa mbaazi, bei imeongezeka kutoka shilingi 1,000 – 1,500 kwa kilo hadi shilingi 2,000 kwa Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi na shilingi 2,200 kwa Mkoa wa Manyara. Bei ya ufuta imeongezeka na kufikia shilingi 4,000 kwa kilo ikilinganishwa na shilingi 1,000 – 1,200 kwa kilo msimu uliopita. Nitoe wito kwa wakulima nchini waendelee kutumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa mazao haya kwa sababu tumeanza kuona tija ya bei nzuri. Hivi karibuni tuliona video ya wananchi kutoka Nanyumbu wakicheza ngoma kushangilia kupatikana kwa bei nzuri ya zao hilo.
Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika (AGRF)
- Mheshimiwa Spika, jana tarehe 7 Septemba, 2023 hapa nchini, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehitimisha Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika (AGRF) lililofanyika jijini Dar es Salaam. Kwenye kongamano hilo walijadili na kuangalia mifumo ya kilimo na namna nchi itakavyoweza kunufaika na kumudu kujiongezea uwezo wa kuwa na chakula cha kutosha na ziada. Jukwaa hilo lilibainisha fursa zitokanazo na kilimo na mijadala hiyo ilihusisha fursa zilizopo kwenye sekta za mifungo na uvuvi katika kutoa fursa za kiuchumi kwa ujumla.
- Mheshimiwa Spika, jukwaa hili kwetu limeleta manufaa makubwa, limekutanisha wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi na kuweza kupeana uzoefu wa namna upatikanaji wa chakula cha kutosha katika kila nchi. Nasi Tanzania tumejikita kwenye eneo hili katika kuhakikisha kwamba jamii yetu inapata chakula cha kutosha.
MASUALA YA USALAMA NA AFYA KAZINI
- , sambamba na kuimarisha sekta ya kilimo, Serikali imeendelea kutekeleza azma yake ya kujenga mazingira bora ya kazi na wafanyakazi. Vilevile, imeendelea kuhakikisha wafanyakazi wanapata stahili zao, vitendea kazi, kufuatilia kwa karibu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi. Hii, ni kutokana na ukweli kwamba masuala ya afya na usalama kazini ni haki ya msingi ya mfanyakazi na yanapaswa kusimamiwa kikamilifu.
- Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kusimamia masuala ya afya na usalama mahali pa kazi kupitia taasisi ya OSHA ambayo ina jukumu hilo kisheria.
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, OSHA imefanya ukaguzi katika maeneo ya kazi 20,067. Ukaguzi huo ni wa usalama wa umeme, mitambo ya kuzalishia mvuke, mitungi ya gesi na hewa, majengo na majenzi, egonomia, zana za kunyanyulia vitu vizito na vipimo vya ubora wa mazingira ya kazi.
- Mheshimiwa Spika, sambamba na kaguzi hizo, OSHA imewezesha maeneo ya kazi kusimika mifumo ya kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokana na mazingira ya kazi. Pia, imesajili maeneo ya kazi 11,036 na kuhamasisha wafanyakazi kupima afya zao kulingana na vihatarishi vilivyomo kwenye kazi wanazozifanya; kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi; kusimamia viwango vya kazi pamoja na masuala ya afya na usalama mahali pa kazi. Lengo ni kuhakikisha Sheria ya Usalama mahali pa kazi inatekelezwa ipasavyo.
- Mheshimiwa Spika, ninayofuraha kulieleza Bunge lako tukufu kuwa kutokana na mafanikio ya OSHA, nchi mbalimbali zimekuwa zikija kujifunza kutoka kwetu. Baadhi ya nchi hizo ni Zimbabwe, Botswana na Kenya. Aidha, hivi karibuni tumepokea maombi ya ugeni kutoka Eswatini na Afrika Kusini watakaokuja kujifunza kutoka kwetu masuala mbalimbali ikiwemo Mfumo wa TEHAMA wa Usimamizi wa Taarifa za Kaguzi nchini (Workplace Inspection Management System – WIMS).
- Mheshimiwa Spika, aidha, ni jambo la kujivunia pia kuona mtaalamu wetu kutoka OSHA ndiye anayesimamia Dawati la Masuala ya Afya na Usalama mahali pa Kazi katika Ofisi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zilizopo Gaborone nchini Botswana. Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu.
- Mheshimiwa Spika, tarehe7 Agosti, 2023 nilipata fursa ya kuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kugawa vitendea kazi na magari 30 ambapo magari 17 ni ya ofisi za mikoa za Idara ya Kazi na 13 ni ya OSHA. Magari hayo na vifaa vya kupima afya na usalama mahali pa kazi vilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 4.3 na vilitolewa ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa ofisi hizo.
- Mheshimiwa Spika, magari hayo 30 yalinunuliwa kwa fedha za ndani ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozitoa katika maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi, 2023 zilizofanyika kitaifa mkoani Morogoro. Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi yake ndani ya kipindi kifupi sana. Na nisisitize watendaji wote kuongeza ufanisi katika utendaji wa kila siku pamoja na kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Usalama na afya mahali pa kazi.
MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI (WCF)
- Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi, Serikali inaendesha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambayo ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263 kwa lengo la kulipa fidia wafanyakazi wanapopata ulemavu au kufariki kutokana na magonjwa au ajali zitokanazo na kazi.
- Mheshimiwa Spika, kama yalivyo madhumini ya kuanzishwa kwake, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi umeendelea kutekeleza kwa ufanisi jukumu la kulipa fidia kwa wafanyakazi waliopata ajali ama magonjwa yanayotokana na kazi. Aidha, Mfuko unalipa fidia kwa wategemezi wao pale ambapo mfanyakazi anafariki kutokana na ajali ya kikazi.
- Mheshimiwa Spika, ulipaji wa fidia umeongezeka kutoka shilingi bilioni 13.19 zilizolipwa kwa mwaka katika kipindi kilichoishia Juni, 2021 na kufikia shilingi bilioni 17.93 kwa mwaka katika kipindi kilichoishia Juni, 2023. Ongezeko hili linaufanya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuwa umelipa jumla ya shilingi bilioni 62.04 kwa wanufaika 11,587 tangu ulipoanza kulipa fidia Julai, 2016 hadi ilipofika Juni, 2023.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na malipo haya, tathmini ya uhai na uendelevu wa Mfuko iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani kwa kipindi cha kuishia tarehe 30 Juni, 2022 imeonesha kuwa Mfuko ni endelevu na uko imara. Aidha, kwa mujibu wa hesabu ambazo zimewasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya ukaguzi hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023, thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 665.06.
HALI YA UCHUMI
Udhibiti wa Mfumuko wa Bei
- Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo hadi kufikia Julai, 2023 mfumuko wa bei umeendelea kupungua na kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 4.5 ya Julai, 2022. Kutokana na jitihada madhubuti na usimamizi wa Serikali, ni matarajio yetu kwamba mfumuko wa bei utaendelea kupungua na kubaki ndani ya lengo, hasa ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa chakula nchini unazidi kuimarika. Tanzania imeendelea kuwa na mfumuko wa bei wa chini ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ukusanyaji Mapato
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Serikali inafikia azma ya kutekeleza utoaji wa huduma kwa wananchi na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati, Serikali imeendelea kuongeza maarifa na matumizi ya teknolojia na mifumo ya TEHAMA kwenye ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vyake mbalimbali.
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilikusanya shilingi bilioni 26,241.8 sawa na asilimia 93.7 ya lengo ikilinganishwa na shilingi bilioni 24,396 mwaka 2021/2022. Kati ya kiasi kilichokusanywa, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 21,411.4, sawa na asilimia 95.6 ya lengo, makusanyo yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 3,845.5, sawa na asilimia 83.5 ya lengo na mapato kutoka vyanzo ya halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 984.9, sawa na asilimia 97.3 ya lengo.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazofanyika katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato, bado kuna changamoto kadhaa ikiwemo ubadhirifu kutoka kwa watumishi wasio waaminifu, kutosomana kwa baadhi ya mifumo na kutokuwa na mifumo imara ya TEHAMA katika baadhi ya taasisi. Kutokana na changamoto hizo za kusimamia na kuimairisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, Serikali imeendelea kutekeleza hatua zifuatazo:
Moja: Kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini katika sekta za uzalishaji ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi;
Mbili: Kutambua na kusajili biashara zisizo rasmi na zinazoendeshwa kidigitali ili kutanua wigo wa mapato;
Tatu: Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kuongeza ulipaji kodi kwa hiari;
Nne: Kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji wa mapato ya ndani; na
Tano: Kudhibiti misamaha ya kodi ili isizidi asilimia moja ya Pato la Taifa.
- Mheshimiwa Spika, Serikali iliundamfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ujulikanao kama TAUSI ili kupunguza urasimu uliokuwepo kwenye ukusanyaji wa mapato. Mfumo huu mpya ni wa kidijitali na humrahisishia mfanyabiashara kufanya malipo ya Halmashauri kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu yake ya kiganjani au kompyuta.
- Mheshimiwa Spika, mfumo huu umelenga kumsaidia mteja kujihudumia mwenyewe, hali ambayo haimlazimu tena kwenda ofisi za halmashauri kuomba au kulipia tozo, ushuru, leseni, faini au vibali mbalimbali. Badala yake anaweza kufanya mwenyewe kupitia dirisha la mteja au Taxpayer Portal.
Kudhibiti Upotevu wa Makusanyo
- Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati kadhaa katika kudhibiti upotevu wa makusanyo ya ndani kwa kutumia mashine za kukusanyia ankara za mapato (PoS). Ili kufikia azma hiyo, Serikali ilisimika mfumo ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya katika halmashauri zote nchini unaojulikana kama TAUSI.
- Mheshimiwa Spika, niwakumbushe watumishi wa umma kuwa bado tunalo jukumu la kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyosisitiza juu ya usimamizi wa ukusanyaji mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati akifunga mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa mjini Kibaha.
- Mheshimiwa Spika, katika hili nawaelekeza wataalamuwetu wa ndani wa mifumo na TEHAMA, wabuni programu tumizi ya kuweza kutambua risiti halali na zisizo halali ili kuweza kujihakikishia kuwa mapato yote yanayokusanywa yanaingia Serikalini. Vilevile, waweke utaratibu wa kufanya kaguzi za kushtukiza kwenye mashine za PoS ili kubaini kama kuna ukiukwaji wowote unaofanyika sambamba na kuwa na utaratibu endelevu wa ufuatiliaji na mfumo wa usalama maalum wa utunzaji taarifa (back-up).
MAELEKEZO MAHSUSI
- Mheshimiwa Spika, wakati naelekea kuhitimisha hotuba yangu naomba sasa nisisitize masuala muhimu yafuatayo:
Moja: Waajiri wachukue hatua za kuimarisha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi wao dhidi ya vihatarishi vilivyomo katika maeneo yao ya kazi. Hatua hizo ni pamoja na kuwa na mwongozo wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kufanya tathmini ya vihatarishi mahali pa kazi, kuhakikisha wafanyakazi wao wanapimwa afya ili kubaini athari ya vihatarishi kwa mfanyakazi na kuhakikisha maeneo yao yanafanyiwa kaguzi za usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi na kulinda uwekezaji wao. Aidha, nitoe wito kwa watumishi wa OSHA wawe waadilifu wanapoendesha mazoezi ya ukaguzi mahali pa kazi na kuchukua vipimo vya wafanyakazi.
Pili: Wafanyakazi wahakikishe wanazingatia taratibu na miongozo ya kujilinda dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali au magonjwa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao. Hii itasaidia kulinda afya na usalama wao pamoja na kumpunguzia mwajiri gharama za uendeshaji pale wanapougua au kupata ajali wakiwa kazini.
Tatu: Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uongeze wigo wa kutoa elimu kwa wafanyakazi ili watambue huduma zinazotolewa na mfuko huo. Vilevile, waajiri watumie ipasavyo mifumo ya TEHAMA kupata huduma, kujisajili na kuwasilisha kwa wakati michango katika mfuko huo.
Nne: Nipende kuwasisitiza wafanyabiashara na watoa huduma watoe risiti halali kupitia mashine za kielektroniki (EFDs) wakati wa mauziano ya bidhaa au utoaji wa huduma kwa wateja. Kwa upande wa wateja, niwakumbushe kuwa ni wajibu wao kudai risiti yenye thamani halisi ya fedha walizotoa.
Tano: Maafisa Masuuli waimarishe usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024;
Sita: Watendaji wa Serikali, waimarishe ukusanyaji wa mapato na kufanya matumizi kwakuzingatia maeneo ya vipaumbele vilivyoainishwa katika bajeti sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Saba: Watumishi wa umma mtenge muda wa kwenda kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao. Wafuateni, wasikilizeni na kutatua kero zao ili wasipoteze muda mwingi kufuatilia lakini pia wasilazimike kwenda ngazi za juu au kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa kwa masuala ambayo mngeweza kuyafanyia kazi.
Nane: Hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watumishi wote wanaosababisha upotevu wa mapato ya Serikali. Nawaelekeza Wakuu wa Mikoa yote kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuwabaini wabadhirifu hao, kuwachukulia hatua mara moja na kutoa taarifa kwa mamlaka.
MICHEZO
- Mheshimiwa Spika, kwa upande wa michezo, nchi yetu imeendelea kupata mafanikio makubwa. Sote tumeshuhudia vilabu vyetu viking’ara katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi. Hivi karibuni tumeshuhudia Timu ya Taifa ya Wasichana Chini ya Miaka 18 (U18) ikichukua ubingwa wa mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) baada ya kuishinda Timu ya Uganda kwa bao moja bila katika mchezo uliofanyika kwenye Viwanja vya Azam Jijini Dar es Salaam.
- Mheshimiwa Spika, ninawapongeza pia, JKT Queens ambayo imefanikiwa kuchukua ubingwa wa CECAFA na hivyo kupata fursa ya kuwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika Mashindano ya Vilabu ya Afrika. Ushindi wa timu hizi za mpira wa miguu za wanawake ni wa kujivunia sana. Nyote mtakubaliana nami kuwa timu za wanawake zimehamasika na zinaendelea kushindana kwa kasi ya juu mno. Ninawatakia kila la heri JKT Queens katika mashindano yanayofuata na nitoe wito kwa wapenzi wa michezo na Watanzania wote kwa ujumla tuendelee kuwaunga mkono ili wazidi kupeperusha bendera ya nchi yetu. Niwasihi waendelee kujifua kwani ushindi ni lazima.
- Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza sana Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ambayo katika mashindano ya Afrika (Africa Games) imeshika nafasi ya tatu na kupata medali ya shaba. Hongereni sana.
- Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchezo wa ngumi almaarufu masumbwi ninawapongeza sana wanamasumbwi walioshiriki katika mashindano mbalimbali. Kipekee nimpongeze Grace Mwakamele aliyetunukiwa medali ya fedha katika mashindano ya ngumi yaliyofanyika Yaounde nchini Cameroon, huyu ni mwanamke wa kwanza Mtanzania kushinda medali ya kimataifa. Pia, ninampongeza bondia Yusuph Changarawe aliyetunukiwa medali ya shaba katika mashindano hayo yaliyofanyika tarehe 25 Julai hadi tarehe 6 Agosti. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitoishukuru Serikali ya India kupitia Ubalozi wake hapa nchini pamoja na Taasisi ya Kalamandalam kwa kuwaunga mkono wachezaji wetu kwani kwa miaka miwili mfululizo wamekuwa wakiandaa hafla maalum ya kuwapongeza na kuwapa zawadi washindi wetu.
- Mheshimiwa Spika, kufuatia mashindano ya Africa Open katika mchezo wa Golf yaliyofanyika nchini Ghana, mchezaji mwanadada shupavu Madina Iddi ameibuka bingwa wa mashindano hayo. Nitumie fursa hii kumpa pongezi nyingi sana kwa ushindi huo mkubwa. Vilevile, niwapongeze wanawake wote wanaothubutu kushiriki katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi. Jitihada zenu tunaziona na kwa hakika mmeendelea kuliheshimisha sana Taifa letu.
- Mheshimiwa Spika, katika michuano ya Klabu Bingwa na Shirikisho Barani Afrika, ninazipongeza sana timu za Yanga, Simba na Singida Fountain Gate kwa kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya pili ya michuano hiyo. Hakika mmeanza vema. Nitumie fursa hii kuwatakia kila la heri katika mashindano yanayoendelea, mpate ushindi mnono na kuweza kuingia hatua ya makundi ili kuzidi kutupa raha Watanzania.
Kipekee, niipongeze Timu ya Simba ambayo imekuwa miongoni mwa vilabu nane bora barani Afrika ambavyo vitashiriki michuano ya African Football League. Michuano hiyo inatarajia kuzinduliwa mwezi Oktoba 2023, Jijini Dar es Salaam. Nawasihi Watanzania kujitokeza kwenye ufunguzi wa michuano hiyo kwani inaitangaza Tanzania kimataifa. Hongera Sana.
- Mheshimiwa Spika, timu yetu ya Taifa au Taifa Stars jana ilishiriki katika mechi ya michuano ya kufuzu kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika (Africa Cup of Nations 2024) yatakayofanyika nchini Ivory Coast. Katika michuano hiyo Tanzania ilihitaji kushinda au kutoka sare ili kuweza kufuzu katika kundi lake. Ninayo furaha sana kuipongeza Taifa Stars kufuzu michuano ya kuwania kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kupambana na Timu ya Taifa ya Algeria huko nchini Algeria. Katika mechi hiyo timu yetu ilitoka suluhu (bilabila) na kuifanya ipate tiketi ya kuendelea na mashindano hayo. Ninaipongeza sana timu yetu ya Taifa na kuitakia kila la heri katika mashindano yajayo. Nami nitumie fursa hii kuwasihi Watanzania wenzangu tuendelee kuwaunga mkono ili wapate hamasa zaidi na kutuletea ushindi.
HITIMISHO
- Mheshimiwa Spika, ninapohitimisha hotuba yangu, nitumie fursa hii kuwashukuru sana watendaji wote wa Serikali ambao wamekuwa chachu kubwa katika kutekeleza masuala ya kitaalamu kwa weledi mkubwa kupitia mipango na ushauri katika kufanikisha shughuli zilizopangwa kwenye mkutano huu. Ninamshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo hasa kwa kuishauri vema Serikali katika kipindi chote cha mkutano huu. Pia, ninamshukuru Katibu wa Bunge na Watumishi wote wa Bunge kwa kuhakikisha wanatupatia huduma nzuri iliyotuwezesha kutekeleza majukumu yetu ipasavyo. Kipekee, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi yao ya kuendelea kusimamia utulivu na amani katika kipindi chote cha Bunge. Ninawashukuru sana wanahabari kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuwahabarisha wananchi yale yaliyokuwa yakijiri kwenye mkutano huu pamoja na madereva waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa bungeni.
- Mheshimiwa Spika, niwatakie Waheshimiwa Wabunge wenzangu safari njema na mnaporejea majimboni kwenu, ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape afya njema na nguvu za kutosha katika kutekeleza wajibu wa kuwahudumia wananchi katika majimbo yenu na maeneo ya uwakilishi mliyopewa dhamana ya kuyaongoza.
- Mheshimiwa Spika, tunatarajia kwamba kati ya tarehe 27 au 28 Septemba, 2023 kutegemea mwandamo wa mwezi kutakuwa na sikukuu ya Maulid. Nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu wote na Watanzania kwa ujumla maadhimisho mema ya mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W).
- Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa ninapenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 31 Oktoba, 2023 saa tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu hapa jijini Dodoma.
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
About The Author
Last modified: September 8, 2023