Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt.Selemani Jafo amesema Serikali inaendelea na jitihada za kumaliza
changamoto ya magugu maji kuzingira Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa
Kilimanjaro.
Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwanga Mhe. Joseph
Tadayo aliyetaka kujua lini Serikali itatekeleza mradi wa kuondoa magugu maji
katika Ziwa Jipe.
Dkt. Jafo amesema Ofisi hiyo kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira (NEMC) tayari zimefanya tathimini ya uharibifu uliopo na
kuandaa andiko la Mradi wa Hifadhi ya Ardhi, na vyanzo vya maji.
Akiendelea kujibu swali hilo amebainisha kuwa jumla ya Dola za Marekani
milioni sita ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 15 zinatarajiwa
kupatikana kupitia mradi huo.
โSerikali imeona changamoto ya uharibifu wa Mazingira unaotokana na kuenea
kwa magugu maji katika Ziwa Jipe, hadi sasa jitihada za kutafuta fedha kutoka
kwa wafadhili mbalimbali zinaendelea,โ amesema Mhe. Jafo.
Amefafanua kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inarejesha ikolojia ya ziwa hilo ili
kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo pamoja na uhifadhi wa
mazingira.
Aidha, Waziri Dkt. Jafo ameongeza kwa kusema kuwa Serikali itahakikisha
inatekeleza mradi huo mara baada ya fedha kupatikana ili kuwanusuru wananchi
wa eneo dhidi ya athari za magugu maji hayo.
Pamoja na majibu hayo pia Waziri Jafo ametoa wito kwa wananchi kuendelea
kuhifadhi mazingira katika Ziwa Jipe ikiwemo kuacha kufanya shughuli za
kibinadamu zisizo endelevu.
Ziwa Jipe lina ukubwa wa kilomita za mraba 30 na linahudumia wananchi zaidi
ya 3,000 wanajishughulisha na shughuli za uvuvi, kilimo, ufugaji na uhifadhi
wa bionuwai pamoja na shughuli za utalii.
Hata hivyo inaelezwa kuwa shughuli za uvuvi zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa
na kukithiri kwa magugu maji yaliyoota ziwani hasa upande wa Tanzania hivyo
Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa magugu maji hayo.
About The Author
Last modified: September 1, 2023