Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Hawa Ghasia (aliyevaa kilemba cha njano ) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI jana walipokagua mradi wa ujenzi na ukarabati wa Soko Kuu la Kariakoo ambapo wameridhishwa na ujenzi wake.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeridhishwa na
kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi wa ukarabati na ujenzi wa soko la Kariakoo
unaotarajia kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu hatua itakayowezesha
wafanyabiashara kurejea.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Lazaro Nyamoga mara
baada ya kukagua mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko la Kariakoo (jana Agosti
27,2023) unaoendelea kutekelezwa na mkandarasi M/s Estim Construction Limited kwa
gharama ya shilingi Bilioni 28.03 zilizotolewa na serikali.
“Ni rai ya Kamati ya Bunge kuwa soko hili ni la kimataifa hivyo Bodi na Menejementi
ziwe na mpango wa uendeshaji soko kimataifa kama ilivyo lengo la Rais Samia Suluhu
Hassan kufuatia kutoa fedha nyingi kujenga na kukarabati mradi huu wa kimkakati kwa
nchi”, alisema Nyamoga.
Nyamoga alitoa ushauri kwa Shirika la Masoko ya Kariakoo kuwa na mfumo wa
ukusanyaji na uchakataji wa taka wa kisasa ili kuepuka kero kwa wafanyabiashara na
kuwa suala la udhibiti wa madalali liwekewe mkakati ili soko litakapofunguliwa wakulima wafanye biashara kwa faida na uwazi.
![](https://www.mwanahabaridigital.co.tz/wp-content/uploads/2023/08/KMC-3-1024x683.jpg)
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI wakipata maelezo kuhusu mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko la Kariakoo jana jijini Dar es Salaam.
Kuhusu ugawaji wa vizimba na maeneo ya biashara, Kamati ya Bunge imeshauri shirika
la Masoko ya Kariakoo kuahakikisha wafanyabiashara waliokuwepo kabla ya soko
kuungua wapewe kipaumbele na kuwepo na uwazi wa waombaji wa nafasi za biashara
hatua itakayosaidia kuondoa malalamiko kwa wananchi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo
Hawa Ghasia, alisema tayari maandalizi ya kuwarejesha waliokuwa wafanyabiashara
wapatao 1,662 yanaendelea ikiwemo kuwahakiki na kuweka mpangilio mzuri wa
biashara na kuwa soko litakapokamilika litakuwa na zaidi ya nafasi za biashara 2,300
zitakazotangazwa kwa umma.
Ghasia aliwaeleza wabunge hao kuwa katika soko jipya la Kariakoo mifumo madhubuti
ya udhibiti wa majanga ikiwemo moto imewekwa pamoja na uwepo wa mifumo ya
kisasa ya Tehama itakayowezesha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha serikali
inapata faida katika mradi huo.
Soko Kuu la Karikaoo ambalo liliungua moto Julai 10 mwaka 2021 linakarabatiwa huku
lililokuwa soko dogo likijengwa upya ambapo litakuwa na ghorofa nane, kati ya hizo
mbili zipo chini ya usawa wa ardhi (basement) na sita juu ya usawa wa ardhi.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ilifanya ziara ya kikazi ya siku tatu jijini Dar
es Salaam kwa kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa na Wakala wa Barabara
za Mijini na Vijini (TARURA), Wakala wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART) na Shirika la
Masoko ya Kariakoo (KMC).
About The Author
Last modified: August 28, 2023