Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kawajika Mwinyipembe akimpima jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) mkazi wa Arusha aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa afya JKCI na wenzao wa MRRH na kumalizika leo Mkoani Kilimanjaro. Jumla ya watu 700 wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Watu 700 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
katika kambi maalum ya siku tano iliyokuwa ikifanywa na madaktari bingwa wa
magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
wenzao wa Hosptiali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH).
Kambi hiyo iliyomalizika jana Mkoani Kilimanjaro imekuwa na mwitikio mkubwa
kuliko ilivyotarajiwa ukilinganisha na uwezo wa mabingwa hao kutoa huduma kwa
watu waliojitokeza.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kufunga kambi hiyo Daktari wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo alisema kupitia kambi hiyo
wameona uhitaji wa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa
ya moyo kwa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani ni mkubwa hivyo kuiomba
Serikali kuangalia namna ya kusambaza huduma hizi na kuzisogeza kwa wananchi.
Dkt. Pedro alisema asilimia 55 ya wagonjwa watu wazima waliowaona walikuwa
na tatizo la shinikizo la juu la damu, huku wengine wakiwa na magonjwa ya kuziba
mishipa ya moyo, magonjwa ya valvu na magonjwa ya umeme wa moyo
kutokufanya kazi vizuri hivyo kuwapa rufaa wagonjwa 70 kufika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete kwaajili ya matibabu zaidi
“Tulichogundua hasa katika jamii ya watu wa Kilimanjaro ni pamoja na watu
wengi kuwa na uzito mkubwa, kuwa na matumizi makubwa ya chumvi na mafuta
mengi lakini pia sababu za kijenetiki za familia kuwa na historia ya kuwa na
magonjwa ya sukari na shinikizo la damu hivyo baadhi ya watu katika familia
kurithi magonjwa hayo”,
“Wito wetu kwa jamii ni kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao pale wanapoona
dalili na wale ambao tayari wana magonjwa yasiyoambukiza wafanye vipimo vya
kuchunguza moyo kwani utakapogundua tatizo mapema matibabu huwa rahisi na
matokeo ya matibabu huwa mazuri zaidi”, alisema Dkt. Pedro
Akizungumza kuhusu watoto waliotibiwa katika kambi hiyo Daktari bingwa wa
watoto kutoka JKCI Parvina Kazahula alisema jumla ya watoto 42 wamefanyiwa
uchunguzi wa magonjwa ya moyo ambapo watoto 16 waligundulika kuwa na
matatizo ya moyo.
Dkt. Parvina alisema watoto 12 walikuwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo
ambayo ni matundu kwenye moyo pamoja na mishipa ya damu inayopeleka damu
kwenye mapafu kuwa na hitilafu, huku watoto wengine wanne wakiwa na
matatizo ya valvu zao za moyo matatizo ambayo wameyapata wakati wa ukuaji.
“Wanawake tunatakiwa kuhudhuria kliniki ili kuweza kufuatilia vitu muhimu
wakati wa ujauzito kupunguza athari za kupata watoto wenye magonjwa ya
moyo, pia watoto wanaozaliwa wakiwa na dalili za magonjwa ya moyo wafikishwe
hospitali mapema ili kuweza kutatua matatizo kwa wakati”, alisema Dkt. Parvina
Dkt. Parvina alisema mtoto anayezaliwa na magonjwa ya moyo huwa na dalili za
ukuaji hafifu, kutokuongezeka uzito, kushindwa kupumua vizuri, kuwa na rangi ya
bluu sehemu za mdomo na vidoleni.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi Dkt.
EdnaJoy Munisi aliwapongeza wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa na
mwitikio mkubwa wa kuchunguza afya zao na kuwataka wananchi hao kuzingatia
ushauri wa wataalamu walioupata katika kambi hiyo.
“Nawaomba wananchi wa Kilimanjaro kuendelea kuwa na tabia ya kupima afya
zenu hata baada ya kambi hii kwani hapa Mawenzi tunayo kliniki ya matibabu ya
magonjwa ya ndani ikiwemo magonjwa ya moyo hivyo msisite kufika kwa ajili ya
kupatiwa matibabu”, alisema Dkt. EdnaJoy
Aidha Dkt. EdnaJoy amewataka wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kupunguza
matumizi makubwa ya chumvi, pombe na nyama nyekundu bali wazingatie ulaji
wa mlo sahihi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya
moyo.
Naye mwananchi aliyepatiwa matibabu katika kambi hiyo Theresia Sangawe
ilishukuru kwa kupata nafasi ya kupima moyo wake katika kambi hiyo na kukutwa
yuko salama.
“Leo nilikuja hapa Hospitali kwa ajili ya kliniki yangu ya shinikizo la damu lakini
nikapata nafasi ya kupima sukari kwenye damu na kupima moyo, nashukuru moyo
wangu umekutwa uko vizuri, kuta za moyo ziko vizuri, na mishipa ya damu pia iko
vizuri”, alisema Theresia
Theresia alisema kambi za matibabu ya kibingwa zikisogezwa kwa wananchi kama
ilivyokuwa ya magonjwa ya moyo kutatoa motisha kwa jamii kuwa na shauku ya
kupima afya zao.
About The Author
Last modified: August 28, 2023