Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akifungua kikao kazi leo jijini Dodoma cha wadau kutoka Serikalini kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi amewataka washiriki katika kikao kazi
cha kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu
kushiriki kikamilifu katika kikao hicho ili kutoa maoni na mapendekezo
yatakayosaidia kuboresha Mfumo huo utakaowezesha kubaini mahitaji
halisi ya watumishi katika Taasisi za Umma.
Bw. Mkomi ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikao
kazi hicho kwa Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu
kutoka Wizara zote, Baadhi ya Makatibu Tawala Wasaidizi wa
Sekretarieti za Mikoa, Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu wa
Halmashauri na Manipaa, Wakurugenzi na Maofisa kutoka OR –
TAMISEMI, Wataalam kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa,
Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Halmashauri za Manispaa.
Sehemu ya wadau kutoka Serikalini wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi wakati akifungua kikao kazi cha wadau hao jijini Dodoma kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.
Bw. Mkomi amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais- UTUMISHI baada ya
kuona tatizo la upungufu wa watumishi katika maeneo mengi iliona
kuna haja ya kutafuta suluhu kwa kutengeneza Mifumo ya kisayansi
itakayosaidia katika uchambuzi wa mahitaji ya watumishi ili kutatua
changamoto hiyo.
Amesema Mfumo mmojawapo uliotengenezwa ni huo wa Tathmini ya
Mahitaji ya Rasilimaliwatu ambao ndio unawasilishwa kwa wadau kwa
lengo la kupata maoni na mapendekezo ya kuboresha ili uwe na tija
kwa ustawi wa taifa, hivyo amewasisitiza kuhakikisha wanajadili kwa
umakini ili Serikali iweze kuondokana na changamoto hii.
Amesema kuwa, kila mwaka Serikali imekuwa ikiandaa ikama lakini
haitoshi kwasababu utaratibu unaotumika ni wa kawaida wa kuajiri
tukifikiri ndio suluhu pekee na kuongeza kuwa ni wakati sasa wa
kuangalia namna ya kufanya, kwani inatakiwa kujua watumishi wangapi
wanahitajika wapi, wakafanye nini na baada ya kujua hayo itapatikana
nafasi nzuri ya kuboresha.
“Kila Mkurugenzi utakayemuuliza atakwambia watumishi hawatoshi,
Mfumo huu wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu utatupa kujua
idadi ya watumishi walioko katika kila kituo cha kazi na upungufu au
ziada iliyopo ili kuwa na idadi ya watumishi sahihi katika sehemu sahihi
za utekelezaji wa majukumu yao.” Bw. Mkomi amesisitiza.
Akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Taasisi, Bw.
Nolasco Kipanda ameelezea lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kupata
maoni toka kwa wadau hao ili kuboresha mfumo huo katika Utumishi wa
Umma kwa masilahi mapana ya taifa.
Kikao kazi hicho kilichoanza leo kinafanyika kwa muda wa siku nne
ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa ili kuwezesha wadau
kuwasilisha maoni sahihi. Mada hizo ni pamoja na Mfumo wa Tathmini
ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu kwa nadharia na vitendo, Uchambuzi
wa Mahitaji ya Watumishi kwa Kuzingatia Uzito wa Majukumu na
Namna ya Kuandaa Majukumu na Viwango vya Kazi
About The Author
Last modified: August 9, 2023