WAGOMBEA 77 kutoka vyama 14 vyenye usajili wa kudumu wameteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwania nafasi wazi za udiwani katika Kata 14 za Tanzania Bara ambazo zinataraji kufanya uchaguzi mdogo Julai 13,2023.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza tarehe 13 Julai, 2023 kuwa siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 14 za Tanzania Bara ambapo uteuzi wa wagombea kwa ajili ya uchaguzi huo umefanyika jana tarehe 30 Juni, 2023.
Wagombea na wananchi wa Kata ya Magubike katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wakitazama fomu za uteuzi za wagombea walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya kubadikwa katika eneo la wazi ili kutoa fursa ya kuweka pingamizi dhidi ya mgombea asiyekuwa na sifa. (Picha na Mroki Mroki-NEC).
Awali Fomu za uteuzi wa wagombea hao zilianza kutolewa kuanzia tarehe 24 Juni, 2023 hadi tarehe 30 Juni, 2023 na jumla ya wagombea 90 walichukua fomu za uteuzi.
Kati ya wagombea hao 90 waliochukua fomu, wanaume walikuwa 74 na wanawake walikuwa 16 lakini hadi dirisha la uteuzi linafungwa saa 10 kamili jioni jana ni jumla ya wagombea 77 waliteuliwa kati ya hao wanaume ni 63 na wanawake ni 14. Aidha, jumla ya wagombea 13 hawakurejesha fomu za uteuzi.
Aidha, Katika kata 13 wameteuliwa wagombea zaidi ya mmoja, huku Kata moja ya Mnavira iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mgombea mmoja tu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ameteuliwa kutokana na wagombea wa vyama vingine kutorejesha fomu za uteuzi.
Wagombea walioteuliwa wanatoka katika vyama vya siasa 17 ambavyo ni AAFP, ACT – WAZALENDO, ADA – TADEA, ADC, CCK, CCM, CUF, DEMOKRASIA MAKINI, DP, NCCR – MAGEUZI, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD na UPDP.
Kwa mujibu wa sharia Ilipofika saa 10:00 Jioni wasimamizi wa uchaguzi walibandika fomu za uteuzi za wagombea walioteuliwa katika eneo la wazi ili watu wanaoruhusiwa kisheria waweze kuweka pingamizi, fomu hizo zitaendelea kubandikwa hadi saa 10:00 jioni leo siku ya tarehe 01 Julai, 2023. Hadi sasa hakuna pingamizi lolote lililopokelewa na wasimamizi wa uchaguzi katika kata zote 14.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kata zinazotarajiwa kufanya uchaguzi mdogo ni pamoja na Ngoywa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Kalola iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Sindeni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Potwe iliyopo Halmashauri ya Muheza, Kwashemshi iliyopo Halamshauri ya Wilaya ya Korogwe, Bosha iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mahege iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Bunamhala iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Nyingine ni, Njoro na Kalemawe zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mnavira iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Kinyika iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Magubike iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Mbede iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo kwenye kata hiyo zitaanza leo tarehe 01 hadi 12 Julai, 2023 na uchaguzi utafanyika tarehe 13 Julai, 2023.
About The Author
Last modified: July 1, 2023