Visit Sponsor

Written by 6:24 pm KITAIFA Views: 96

HAKUNA MAHALI POPOTE TPA ILIPOSAINI MKATABA WA MIAKA 100-MKURUGENZI

KINACHOENDELEA katika mitandao ya kijamii nchini juu ya upotoshwaji wa kile kinachodaiwa kuchukuliwa kwa Bandari ya Dar es Salaam na kumilikishwa kwa kampuni ya DP World (DPW) kutoka Falme za Kiarabu (UAE), ni kutokanan na kukosa uelewa juu ya suala halisi.
Katika hali ya kushangaza kwa kukusudia au kwa kutokujua baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa na wanaojiita wanaharakati wamekuwa wakieleza habari za upotoshaji ikiwemo suala la mkataba wa miaka 100, ambapo hakuna mahali popote palipowahi kutajwa kuchukuliwa kwa bandari kwa muda huo.
Jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa alitoa taaraifa kwa waandishi wa habari akifafanua upotoshaji huo akibainisha kuwa taarifa zinazosambaa si sahihi na kwamba zinatengenezwa makusudi na watu wenye nia ovu.
“TPA  inapenda kuwajulisha wateja, wadau wa kitaifa na kimataifa na umma kwa ujumla kwamba taarifa hizo si sahihi, ni upotoshaji unaofanywa kwa makusudi na watu wenye nia ovu ya kukwamisha mipango thabiti ya nchi katika kuongeza ufanisi wa sekta ya bandari nchini kwa maslahi mapana ya taifa,” alisema Mbossa.
 Aidha, alibainisha kuwa taarifa sahihi ni kuwa kilichopo ni makubaliano baina ya serikali mbili za Tanzania na UAE wenye ukomo wa miezi 12 kwa ajili ya kutoa nafasi kujadiliana kuhusu maeneo ambayo Serikali hizo mbili zinaweza kushirikiana katika boreshaji na endelezaji wa sekta ya bandari nchini.
Ushirikiano huo lengo lake ni kuongeza ufanisi wa bandari nchini, kukuza ajira za Watanzania na kufungua fursa za uwekezaji kwenye baadhi ya maeneo ya Bandari ya Dar es Salam kiuchumi na viwanda (Special Economic and Industrial Zones).
 Maana yake, hata uwekezaji katika mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka bandari za ndani na nchi za jirani ambazo zinatumia bandari zilizopo nchini utaimarika kutokana na kuboreshwa huduma na uharaka wa utoaji mizigo hasa makontena.
 “Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inawaomba wateja kutambua kwamba, jitihada zote na hatua zinazochukuliwa na Serikaliya Awamu ya Sita katika kuvutia uwekezaji nchini hususan kwenye maeneo ya bandari zinalenga kumaliza changamoto za muda mrefu ikiwemo ucheleweshwaji wa meli, mizigo, ufanisi katika Bandari zetu,” alisema Mbossa.
 Itakumbukwa Rais Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara katika Falme za Kiarabu (UAE) wakati wa tamasha la Dubai Expo 2020 mnamo Februari 2022 ambapo alipata wasaa wa kukutana na kiongozi wa Dubai wakafanya mazungumzo juu ya fursa zilizopo nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo ambayo Rais Samia aliambatana na mawaziri kadhaa na viongozi wa taasisi mbalimbali ikiwemo TPA, baadhi ya makubaliano yaliyoingiwa ni pamoja na makubaliano ya pande mbili (Memorandum of Understanding – MoU) baina ya TPA na DP World, mnamo Februari 28, 2022.
MoU hiyo ililenga ushirikiano baina ya TPA na DP World katika maeneo kadhaa ikiwemo uendelezaji miundombinu ya baadhi ya bandari za bahari na maziwa nchini, kuongeza ufanisi wa huduma katika bandari na kuimarisha korido za biashara, ubinifu na kuimarisha kanda maalum za kibiashara (Special Economic Zones).
Kwa mujibu wa mwanahabari wa muda mrefu ambaye hakutana kutajwa jina lake gazetini, ameeleza kuwa kilichosainiwa ni kitu kinachotwa IGA, Inter-Governmental Agreement.
“Hii IGA inadumu kwa miezi 12 kuanzia iliposainiwa. IGA imesainiwa kuruhusu mchakato wa kujadili mkataba na masharti ya uendeshaji chini ya HGA – Host Government Agreement. Kwa msingi huo hakuna mahali popote palipotajwa neno miaka 100, hata sijui wametoa wapi,” alisema mwanahabari huyo ambaye alifafanua kuwa hata Tanzania hakuna sharia inayoruhusu wageni kumiliki ardhi kwa miaka 100. Miaka inaishia 99 na si zaidi.
Vilevile, katika maelezo ya Mkurugenzi wa TPA, Plasduse Mbossa: “Naomba kuwataarifu kwamba kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa Bandari Sura 166 ya mwaka 2004, TPA ni mmiliki, msimamizi, mwendeshaji na muendelezaji wa maeneo ya bandari nchini. 
 “Kwa mujibu wa sheria hii TPA itabaki kuwa hivyo hata pale ambapo kutakuwa na wawekezaji katika baadhi ya maeneo ya Bandari. Majukumu ambayo TPA imekuwa ikikasimisha kwa sekta binafsi ni uendeshaji na uendelezai wa baadhi ya maeneo ya Bandari zake kama ambavyo imekuwa ikifanyika huko nyuma. 
 “Kwa ujumla na kwa mujibu wa Sheria ya Bandari, TPA itaendelea kuwepo na kuendelea kutekeleza majukumu yake ya umiliki, usimamizi, undeshaji na uendelezaji wa shughuli za kibandari nchini.”
 Alikumbusha kuwa Kampuni ya Upakuaji Mizigo ya TICTS ambayo ilifanya kazi na bandari hiyo kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2022, ilikuwepo bandarini kwa takribani miaka 22 hakujawahi kuwa na changamoto yoyote ya ulinzi na usalama huku TPA ikiendelea na usimamizi wake kwa mujibu wa sheria.

About The Author

(Visited 96 times, 1 visits today)

Last modified: June 8, 2023

Close