Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Jane Mathew akimpima kiwango cha sukari kwenye damu mtoto aliyefika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.
Watu 335 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwenye kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili iliyomalizika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt.Tulizo Shemu alisema matibabu hayo ya tiba mkoba yajulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ilifanyika maalumu kwaajili ya kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakitoa ushauri
wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za moyo
na lishe bora kwa wananchi waliofika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya
kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya
matibabu iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.
Dkt. Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema katika kambi hiyo watu waliowaona walitoka ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam na wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu pamoja na matatizo mengine ya moyo.
“Nusu ya watu tuliowaona walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na wengine walikuwa na matatizo ya kutanuka kwa moyo, mishipa ya damu ya moyo kuziba, mafuta mengi kwenye mishipa ya damu, maumivu ya kifua, shida za valvu, shida ya mfumo wa umeme wa moyo pia tumewaona watoto waliokuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa kwenye mpangilio wake”,.
“Tuliowakuta na shida za moyo na wengine waliokuwa na shida mbalimbali za mwili kama vile masikio, mifupa, ngozi, macho tumewapeleka katika kliniki zetu kwaajili ya matibabu kwani katika hospitali hii licha ya kutibu moyo tunatibu pia magonjwa mengine pia wengine tumewapa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)”, alisema Dkt. Shemu.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali
ya Dar Group Flaviana Masegesa na Afisa Masoko wa Hospitali hiyo Ireen Mbonde wakichukuwa taarifa mbalimbali wakati wa zoezi la uchunguzi na matibabu ya
moyo lililomalizika jana katika Hospitali hiyo.
Dkt. Shemu alisema kambi za aina hiyo zitakuwa zinafanyika mara kwa mara katika Hospitali hiyo kwani kwa kufanya hivyo wananchi wengi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani watafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Kwa upande wao wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kuomba iwe endelevu ili watu wengi zaidi waweze kufikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Tatu Hassan mkazi wa Shinganya alisema aliona katika TV tangazo la kufanyika kwa matibabu hayo na kuchukuwa hatua ya kwenda kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo.

Watafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) makao makuu na Hospitali ya Dar Group wakichukuwa taarifa za wananchi waliofika katika Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana.
“Ninaishukuru Serikali kwa kutuangalia wananchi wanyonge wenye kipato cha chini na kutufikishia huduma hii ya matibabu ya kibingwa. Nimefika hapa nimefanyiwa vipimo, nimepewa ushauri na dawa za kwenda kutumia mwezi mmoja kwani mimi ninatatizo la shinikizo la juu la damu ambalo limepelekea moyo wangu kutanuka”, alisema Tatu.
“Ninatoa wito kwa wananchi wenzangu wanapoona matangazo ya upimaji wa magonjwa mbalimbali wasipuuze wawahi hospitali mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu mapema kuliko kusubiri hadi waumwe ndipo waende kutibiwa”, alisema Richard John mkazi wa Tegeta.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo kwa kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Hadi sasa wameshatoa huduma hiyo katika mikoa 12 na kuona watu 7196 ambapo 847 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo.
About The Author
Last modified: September 4, 2023